• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Baraza la usalama la UM lapitisha azimio la kukomesha migogoro barani Afrika

    (GMT+08:00) 2019-02-28 09:22:55

    Baraza la usalama la umoja wa mataifa limepitisha azimio kuonesha utayari wa kuchangia juhudi za Umoja wa Afrika "kukomesha vita zote kabla ya mwaka 2020" na "kufikia lengo la kuwa na Afrika isiyo na migogoro". Azimio hilo nambari 2457 lililopitishwa kwenye mkutano wa wazi wa umoja wa Afrika kuhusu kukomesha migogoro barani Afrika, linatambua kuwa kazi ya kujenga Afrika isiyo na migogoro iko mikononi mwa Umoja wa Afrika, nchi wanachama, watu wake na taasisi zake, pamoja na jumuiya zisizo za kiserikali.

    Azimio hilo limeelezea uungaji mko wake kwa juhudi za Afrika kutafuta masuluhisho ya Afrika kwa matatizo ya Afrika, huku likitambua umuhimu wa jumuiya ya kimataifa na ushirikiano, kusaidia kuharakisha mchakato wa kufanikisha lengo la kuwa na amani. Azimio hilo pia limesisitiza haja ya kuwepo kwa njia zenye ufanisi za kutekeleza udhibiti wa silaha, kunyang'anya silaha na kutekeleza vikwazo vya silaha vilivyopitishwa na Baraza la usalama la Umoja wa mataifa.

    Kamishna wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia maswala ya kukomesha migogoro kabla ya mwaka 2020 Bw. Ramtane Lamamra, amesema wakati mwezi Desemba mwaka kesho ambayo ni tarehe ya mwisho ya kukomesha migogoro inapokaribia, ni muhimu kutambua kuwa bado kuna changamoto nyingi na vizuizi vinavyokwamisha Afrika kuwa na mazingira ya kupata maendeleo halisi na kunufaika na amani.

    Ofisa mwandamizi anayeshughulikia mambo ya Afrika kwenye wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini, Bw Mxolisi Nkosi, amesema Afrika Kusini inaamini kuwa Afrika isiyo na vita na yenye amani, ni muhimu katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030, na ajenda ya Umoja wa Afrika kuelekea mwaka 2063. Amesema mpango wa utekelezaji wa kutokomeza vita kabla ya mwaka 2020, na utaratibu wa kufuatilia vitafafanuliwa zaidi kwenye baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika.

    Akiongea kwenye mkutano huo, naibu mjumbe wa kudumu wa China kwenye baraza la usalama la Umoja wa mataifa balozi Wu Haitao, ameitaka jumuiya ya kimataifa kuisadia Afrika kujenga uwezo wa kulinda amani na usalama, na kutoa mwito wa kuwepo kwa ushirikiano wa karibu zaidi kati ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa na baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika ili kuleta amani. Amesema jumuiya ya kimataifa inaweza kusaidia kuondoa vyanzo vya migogoro barani Afrika, kwa kuongeza misaada ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ametaja maeneo ya kipaumbele yanayohitaji msaada kuwa ni kilimo, afya, elimu, uchumi na biashara na miundombinu, ili kuisaidia Afrika kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia. Pia amezihimiza nchi za Afrika kupunguza umaskini, kuendeleza uchumi na kuboresha maisha ya watu, ili kuongeza uwezo wa nchi hizo kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.

    Na mjumbe wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa mataifa Bw. Lazarus Amayo, ametaja mambo matatu muhimu yanayoweza kusaidia kutokomeza migogoro ya kivita barani Afrika. Kwanza ni kuondoa vyanzo vya migogoro hiyo, pili ni kuhimiza ushirikiano wa kitaifa na kimataifa, na tatu ni kujenga uwezo kwa nchi za Afrika kutekeleza mikataba ya kimataifa. Pia amesema wadau wa maendeleo wa nchi za Afrika, wanatakiwa kusimamia vizuri biashara ya silaha kutoka kwenye vyanzo ili kuzuia silaha kwenda kwenye maeneo yenye migogoro.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako