Huu ni mwaka wa 5 tangu China itoe pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja". Waziri mkuu wa China Bw. Li Keqiang hivi karibuni alipotoa ripoti ya kazi za serikali aliagiza kuendelea kusukuma mbele ujenzi wa pendekezo hilo. Na pendekezo hilo pia limefuatiliwa na wajumbe wa Baraza Kuu la Mashauriano ya kisiasa.
Katika miaka ya hivi karibuni, mashirika ya China yameanzisha maeneo mengi ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara katika nchi za nje. Hii ni njia nzuri inayoungwa mkono na serikali za pande mbili kwa ajili ya kupata mafanikio ya pamoja. Mjumbe wa Baraza la Mashauriano ya kisiasa la China Bw. Li Jianhong, ambaye pia ni mkuu wa Shirika la Merchants la China CMG amesema, kuanzisha maeneo ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara katika nchi zilizojiunga na pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja" ni dalili ya China kufungua mlango zaidi na kujitahidi kupata maendeleo ya pamoja na dunia nzima. Ameongeza kuwa kutokana na hali mpya, maeneo hayo yanahitaji kuinuliwa kiwango na kupewa majukumu mapya. Anasema,
"Jambo la kwanza tunalozingatia ni kupata njia ya kuzisaidia nchi hizo kuendeleza uchumi, kuboresha maisha ya watu na kuongeza ajira kutokana na hali zao. Na jambo la pili tunalofikiria ni kupata kiasi kinachofaa cha faida, kwani sisi ni makampuni, hatuwezi kuendelea na shughuli bila faida yoyote."
Bw. Li ameeleza kuwa shirika la CMG kwa kutumia uzoefu wake liliopata katika miaka 40 iliyopita nchini China, limeendeleza vizuri maeneo ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara yaliyoanzishwa nalo nchini Djibouti na Sri Lanka.
Ikiwa njia muhimu ya ushirikiano wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja", kujenga maeneo ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kunahitaji mitaji mikubwa na muda mrefu. Mjumbe wa Baraza la Mashauriano ya kisiasa la China Bw. Zhang Zhanbin, ambaye pia ni mkurugenzi wa idara ya uchumi ya Chuo cha Siasa cha China amependekeza kuwa, idara zinazoshughulikia mambo ya fedha za China zinapaswa kutunga sera chanya ili kutatua tatizo la mitaji linaloyakabili makampuni ya China yaliyoko nje ya nchi. Anasema,
"Baada ya kufanya utafiti katika maeneo ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara yaliyoanzishwa na mashirika ya China katika nchi za nje ikiwemo Eneo la Viwanda la Mashariki la Ethiopia, niligundua kuwa ujenzi wa maeneo hayo pia unahitaji uungaji mkono wa kifedha, na msaada wa Benki ya Upanuaji ya China na Benki ya Exim ya China ni muhimu kwao. Katika miaka ya hivi karibuni, tumefanya kazi nyingi, lakini bado hazitoshi. Baadaye tunapaswa kutafuta njia ya kutoa msaada zaidi ambayo inaweza kuhakikisha usalama wa mitaji na ufanisi wa matumizi ya fedha."
Mjumbe wa Baraza Kuu la Mashauriano ya kisiasa la China Bw. Wang Jianyi, ambaye pia ni mkuu wa Shirika la Futong ametoa pendekezo la kuharakisha kutunga sheria ya kuhimiza uwekezaji katika nchi za nje. Anasema,
"Sasa ni wakati mzuri wa kutunga sheria ya kuhimiza uwekezaji katika nchi za nje. Kutokana na ongezeko la uwekezaji wetu katika nchi za 'Ukanda Mmoja, Njia Moja', ni muhimu kwa makampuni ya China kupata ulinzi wa kisheria."
Bw. Wang amesema kuwa sheria hiyo si kama tu itaweza kuratibu makampuni ya China na nchi yaliko, bali pia itasaidia kujenga mfumo wa dhamana yw makampuni hayo, ili kuhimiza ujenzi wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja".
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |