Katika miaka 6 tangu China itoe pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja", miradi mingi imetekelezwa katika nchi zilizojiunga na pendekezo hilo. Miradi hiyo imehimiza maendeleo ya uchumi wa nchi hizo, na pia kuzisaidia kuongeza uwezo wa kupata maendeleo zaidi. Katika siku zijazo, China itaongeza ushirikiano wa kibiashara katika miradi mikubwa ya pendekezo hilo.
Huu ni mwaka wa sita tangu China itoe pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja". Mkurugenzi wa idara ya uchumi wa kimataifa ya wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Wang Xiaolong amesema, katika miaka 6 iliyopita, maoni ya pamoja kuhusu pendekezo hilo yanaongezeka. Anasema,
"Hadi sasa, jumla ya nchi 123 na mashirika 29 ya kimataifa zimesaini makubaliano ya ushirikiano wa 'Ukanda Mmoja, Njia Moja' na China. Katika miaka 6 iliyopita, miradi mingi ya miundombinu ya kuungana imetekelezwa katika nchi zilizojiunga na pendekezo hilo, na kutia nguvu kubwa kwa maendeleo ya uchumi wa nchi hizo na China. Mchango wa miradi ya ushirikiano wa sekta za uchumi pia umedhihirika, haswa katika kuongeza hadhi ya nchi zilizotekelezwa miradi hiyo kwenye mnyororo wa uzalishaji na utoaji wa bidhaa duniani, na kuongeza nguvu ya ndani ya maendeleo ya nchi hizo."
China inafuata kanuni ya kujadiliana, kujenga na kunufaika kwa pamoja katika ujenzi wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja", na pia inaheshimu utaratibu wa soko. Meneja mkuu wa idara ya masoko ya Kampuni ya Ujenzi wa Umeme ya Shangdong Bw. Zhu Lintao amesema, kituo cha uzalishaji umeme kwa mafuta na kusafisha maji ya chumvi kilichojengwa na kampuni hiyo nchini Saudi Arabia kinaweza kuzalisha umeme megawati 16,800 kwa mwaka, na maji ya kunywa yanayoweza kutosheleza watu laki nne. Bw. Zhu amesema kampuni hiyo ilitumia njia ya kimataifa ya zabuni na uendeshaji katika ujenzi wa miradi hiyo, na kushirikisha makampuni mbalimbali kutoka Ujerumani, Hispania, Marekani na Korea ya Kusini.
Naibu katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Maendeleo na Mageuzi ya China Bw. Zhou Xiaofei amesema, katika siku zijazo, China itaendelea kufanya ushirikiano wa kibiashara na pande nyingine katika miradi mikubwa ya "Ukanda Mmoja, Njia Moja". Anasema,
"Tunakaribisha makampuni ya nchi zilizojiunga na pandekezo la 'Ukanda Mmoja, Njia Moja' na nchi zilizoendelea, pamoja na makampuni makubwa ya kimataifa kushiriki kwenye ujenzi wa pandekezo hilo, ili kupata mafanikio ya pamoja."
Aidha Bw. Zhou amesema China pia itaendelea kuimarisha huduma ya kifedha kwa ajili ya ujenzi wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja", na kutaka kushirikiana na makampuni ya kimataifa ya kifedha kujenga mfumo tulivu, endelevu, wenye uwezo wa kudhibiti hatari na wa muda mrefu wa uwekezaji kwa ajili ya ujenzi huo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |