• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yapiga hatua katika kubana matumizi ya maji

    (GMT+08:00) 2019-03-22 18:16:32

    Leo ni siku ya maji duniani. China ina idadi kubwa ya watu na maliasili chache ya maji, hivyo inatekeleza mfumo mkali wa kudhibiti matumizi ya maji. Naibu waziri wa maji na umwagiliaji wa China Bw. Wei Shanzhong amesema, China imepiga hatua chanya katika kuhimiza kubana matumizi, kuhifadhi na kusimamia maliasili ya maji, huku ikiharakisha kushughulikia suala la matumizi ya kupita kiasi ya maji yaliyoko chini ya ardhi katika sehemu ya kaskazini.

    Kwenye mkutano na waandishi wa habari wa ofisi ya habari ya baraza la serikali la China, naibu waziri wa maji na umwagiliaji wa China Bw. Wei Shanzhong amesema, katika miaka ya hivi karibuni, China imechukua hatua za kudhibiti idadi na kasi ya matumizi ya maliasili ya maji, na kupata mafanikio dhahiri. Anasema,

    "Tangu China ianze mpango wa 13 wa miaka mitano ( kati ya mwaka 2016 hadi 2020 ), imedumisha utulivu wa kiasi cha jumla cha matumizi ya maji, ambacho kimedhibitiwa kuwa ndani ya tani bilioni 610. Ikilinganishwa na mwaka 2012, matumizi ya maji kwa kila uzalishaji mali wa yuan elfu 10, yamepungua kwa asilimia 30."

    China inasukuma mbele ujenzi wa jamii inayobana matumizi ya maji kwa njia mbalimbali, zikiwemo kufanya mageuzi ya kiteknolojia katika sekta zinazotumia maji mengi, kuboresha mtandao wa mabomba ya maji mijini, na kuongeza matumizi ya maji yasiyo ya kawaida. Wakati huohuo, China imefanikiwa kuongeza uwezo wa kugawanya na kuhamisha maliasili ya maji, na mradi wa kusafirisha maji ya kusini kwenda kaskazini umetoa tani bilioni 23 za maji kwa sehemu zinazokumbwa zaidi na upungufu wa maji ikiwemo miji ya Beijing na Tianjin, na mikoa ya Hebei na Henan.

    Bw. Wei amesema sehemu ya kaskazini ya China inaathiriwa zaidi na upungufu wa maji, na imetumia maji yaliyoko chini ya ardhi kupita kiasi. Anasema,

    "Sehemu ya kaskazini ina watu milioni 168, na asilimia 4 ya maliasili ya maji. Hivyo imechukua maji yaliyoko chini ya ardhi kwa kupita kiasi. Baadhi ya maji hayo yana fluorine nyingi, na kuweza kuleta athari mbaya kwa afya ya watu na mazingira."

    Mwaka jana, China ilijaribu kurudisha maji chini ya ardhi mkoani Hebei kwa kutumia maji yaliyohamishwa kutoka sehemu ya kusini. Hivi karibuni, wizara ya maji na umwagiliaji imeagiza kuharakisha kushughulikia suala la matumizi ya kupita kiasi ya maji yaliyoko chini ya ardhi. Bw. Wei anasema,

    "Kuna pengo kubwa, na kazi hii itachukua muda mrefu. lengo letu ni kwamba, hadi mwaka 2022, kama hali ya mvua itakuwa ya kawaida, tutapunguza matumizi ya maji yaliyoko chini ya ardhi kwa asilimia 70 katika miji ya Beijing, Tianjin na mkoa wa Hebei, na hadi mwaka 2035, tutatatua kabisa suala la matumizi ya maji yaliyoko chini ya ardhi."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako