• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Utafiti wa kilimo kati ya Kenya na China kutatua changamoto za upungufu wa Chakula

    (GMT+08:00) 2019-04-24 08:48:34

    Kwenye ripoti mfululizo leo kuhusu ushirikiano wa wataalam na wasomi wa China na Kenya, Ronald Mutie anaripoti kuhusu kazi za maabara ya pamoja ya kilimo kwenye Chuo kikuu cha Jomo Kenyatta cha kilimo na Teknolojia. Maabara hiyo imejengwa kwa msaada wa China kupitia chuo kikuu cha sayansi cha China. Hii hapa ripoti yake.

    Kama ilivyo nchi nyingi za Afrika kilimo kinasalia kuwa tegemea kubwa la kiuchumi.

    Lakini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa shughuli za kilimo katika baadhi ya nchi zimeathrika na kusababisha pia kupungua kwa chakula. Na kuwaacha wakulima bila matumaini.

    "Nimepata hasara kubwa sana, miti yote imekauka." Anasema mmoja wa wakulima kaskazini mwa Kenya.

    Nchini Kenya kwa mfano kiangazi cha mara kwa mara husababisha baa la njaa hasa kwenye kaunti kame za mashariki na kaskazini.

    Kwenye ripoti hii tunazungumza na Profesa David Mburu wa Chuo kikuu cha Jomo Kenyatta cha kilimo na Teknolojia, kwanza anaelezea hali ya kilimo nchini humo.

    "Tatizo kubwa tulilonalo nchini Kenya ni mavuno machache. Hali hii inatokana na sababu kadhaa kama vile mabadiliko ya hali ya hewa na kupungua kwa mvua. Pia tuna changamoto za wadudu na athari zao kwa mimea ya vyakula. Tunahitaji pia kuwa na mbegu ambazo zinaweza kuhimili kiwango fulani cha kiangazi na zenye kukomaa mapema. Tunahitaji pia teknolojia za kilimo ambazo zitawezesha kupata mavuno."

    Lakini sasa ushirikiano kwenye utafiti wa kilimo kati ya Chuo kikuu cha Jomo Kenyatta cha kilimo na Teknolojia na kile cha sayansi cha China umefanikiwa kutatua baadhi ya changamoto hizi.

    Wasomi wa vyuo hivyo viwili wamekuwa wakishirikiana kutafiti teknolojia za kisasa.

    "Tunashirikiana na Chuo kikuu cha sayansi cha China na tunafanya utafiti na wataalam kituo cha kilimo na biolojia ya mazingira. Pia tunashirkiana na chuo kikuu cha Lazhou. Kwenye vyuo vyote viwili tuna wanafunzi wa Chuo kikuu cha Jomo Kenyatta cha kilimo na Teknolojiawanaosomea Uzamili huko."

    Baada ya kufanyia majaribio kwenye shamba la Chuoni, Profesa Mburu anasema wanapeka teknolojia hiyo hiyo nyanjani ili kutathmini utendaji wake.

    Lengo la utafiti wao hasa ni kuwezesha wakulima kutumia raslimali chache na ardhi ndogo, lakini kuzalisha chakula cha kutosha.

    "Pia tunapeleka teknolojia yetu kwa wakulima na tunafanya hivyo kwa kushirikiana na vituo vya mafunzo ya kilimo na pia kupitia wizara za kaunti. Katika vituo vyamafunzo ya kilimo, wakulima wanakuja kujifunza teknolojia na tunaamini mafunzo hayo yatakuwa na athari."

    Akiwa kwenye ziara nchini China, Profesa Mburu alijonea teknolojia ya kutunza maji kwenye udongo ambayo inasaidia mimea kunawri hata kwenye maeneo kame.

    Baada ya kuifanyia majaribio kwenye chuo, waliijaribu pia katika mashamba ya wakulima sehemu mbalimbali nchini Kenya na kusaidia kuimarisha mavuno.

    "Mojawepo wa teknolojia ambazo wakulima wa china wameitumia na ambayo imeongeza mavuno yao kwa kiasi kikubwa ni kutumia plastiki nyembamba kufunika udongo. Teknolojia hii inahusisha plastiki nyembamba ili kuzuia kupotea kwa unyevu kwenye udongo baada ya mvuaTumejaribu teknolojia hii kwenye chuo chetu hapa JKUAT na pia tumeijaribu katika maeneo kame kama vile Machakos na Kituo na matokeo yake yanatia moyo."

    Ushirikiano kati ya vyuo hivi viwili ulianzishwa mwaka wa 1999 na matokeo yake yamekuwa ni ufadhili wa kujenga na kuweka vifaa kwa maabara 6 kwenye chuo kikuu cha Jomo Kenyatta.

    Ufadhili huo umetolewa na serikali ya China kupitia chuo kikuu cha sayansi cha China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako