• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wananchi wa Uganda wanufaika na msaada wa madaktari kutoka China

    (GMT+08:00) 2019-04-30 08:45:12

    Msaada wa matibabu wa China barani Afrika una historia ndefu.Mwaka 1963 China ilituma madaktari 100 nchini Algeria baada ya kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa.Hata hivyo kiwango cha misaada ya kimatibabu kimekuwa kikiongezeka katika nchi mbalimbali kadri siku zinavyosonga.

    Uganda ni mojawapo ya nchi zinazonufaika na msaada wa madaktari kutoka China kwa zaidi ya miongo mitatu sasa.

    Msaada huu umewawezesha maelfu ya wananchi wa Uganda kupata matibabu maalum kutoka kwa wataalamu wa magonjwa mbalimbali kutoka China.

    China imekuwa ikitoa msaada wa dharura wa kimatibabu barani Afrika. Kati ya mwaka 2013 na 2016,zaidi ya watu 11,000 walipoteza maisha yao wakati wa mlipuko wa ugonjwa hatari wa ebola.China ilituma zaidi ya wataalamu wa matibabu 1000 magharibi mwa Afrika,na kutoa msaada wa $120 milioni (750m RMB).

    Nchini Uganda madaktari wa China wamekuwa wakitoa misaada tangu miaka 35 iliyopita.Timu ya madaktari wa China nchini Uganda ina historia ndefu.

    Hapa jijini Kampala katika kijiji cha Wakaliga nimekutana na mzee Godfrey Walakira Mpagi ambaye wakati wa ujana wake alikuwa na matatizo ya ugonjwa wa moyo lakini alipata msaada wa matibabu kutoka kwa madaktari wa China ambao walikuwa katika hospitali ya Kabalagala.

    "Jina langu ni Godfrey Walakira kutoka kijiji cha Wakaliga.Nina umri wa miaka 56 .Naweza kusema kuwa madaktari wa China ni wazuri sana na kusema ukweli dawa zao ni bora.Ukitumia dawa za madaktari wa China na madaktari wengine utaona kuwa dawa za China ni nzuri sana.Nilikuwa na matataizo ya moyo nikaenda kuwaona madaktari wa China na sasa niko sawa,nimepona"

    Mzee Walakira anasema madaktari wa China wamemsaidia sana kwani baada ya kupona ugonjwa wa moyo,alipatikana na vidonda vya tumbo miaka saba iliyopita.Anasema alirudi tena kwa madaktari wa China.

    "Nilikuwa na vidonda vya tumbo nilienda tena hospitali ya Kabalagala,kulikuwa na madkatari wa kutoka China,walinipatia dawa nikapona.Nafikiri sasa yapata kama miaka sita saba nimekuwa nikitumia dawa za madkaktari wa China,dawa hizo ni nzuri sana."

    Aidha Mzee Walakira anasema China imewanufaisha sio yeye tu bali watu wengi nchini Uganda.

    "Naweza kusema kuwa wachina wametoa mchango mkubwa sana kwa watu wetu hapa.Mimi ni mfano.Wamenisaidia sana hivi sasa ni mzima na mwenye afya."

    Wananchi wa Uganda wananufaika na juhudi za serikali ya China za kuboresha mfumo wa kitaifa wa utoaji huduma za afya nchini humo. Hospitali ya Urafiki kati ya China na Uganda,yaani China-Uganda Friendship Hospital Naguru inatoa huduma za matibabu kwa mamia ya wananchi wa Uganda kila siku bila malipo yoyote.

    Caroline Nanyonjo ni mmoja kati ya wengine wengi ambao wanakuja kupata huduma za matibabu katika hospitali hii ya China-Uganda Friendship Hospital Naguru.

    Bi Nanyonjo alikuja hospitalini hapa na kujifungua kwa njia ya upasuaji.

    "Nilijifungua salama kupitia upasuaji.Mtoto wangu yuko salama ,hata mimi pia naendelea vizuri."

    Mkurugenzi wa hospitali ya Urafiki kati ya China na Uganda Naguru ,Dkt Emmanuel Batiibwe anasema wameweza kupunguza vifo vya watoto na mama wanapojifungua kwa asilimia 99.

    "Tumewafanyia upasuaji wagonjwa zaidi ya 7,000 na kuwazalisha mama waja wazito zaidi ya 22,000 kila mwaka .Na katika kufanya hivyo tumeweza kuwa na asilimia 99.7 ya wote tunaowahudumia kurudi nyumbani hai na bora kuliko walivyokuja".

    Hospitali ya China-Uganda Friendship Naguru ilifunguliwa rasmi Januari mwaka 2012.Ilifadhiliwa na China,ilijengwa na China na kuwekwa vifaa na China ,kwa gharama ya $8 milioni.

    Serikali ya China haikukomea hapo,ilileta madaktari bingwa na kuahidi kuendelea kuifadhili hospitali hii ya Urafiki kati ya China na Uganda ya Naguru kama anavyoeleza Mkurugenzi Dk Emmanuel Batiibwe.

    "Tulisaini itifaki katia ya serikali ya Uganda na serikali ya China.Katika mkataba huu tulikubaliana kwamba serikali ya China itakuwa ikitupa idadi ya madaktrai wataalamu kila mwaka ,na watakuwa wakiwalipa,na kuwasafirisha hapa.Kwa upande wetu tutawapokea hapa,tuwape uhuru wa upatikanaji wa matibabu,malazi na usafiri kwa kipindi ambacho wako hapa.Katika mkataba huo pia tulikubaliana kuwa serikali ya China itakuwa ikitupatia msaada wa madawa na vifaa vya matibabu wa gharama ya Ushs 0.3 bilioni kila mwaka"

    Serikali ya China imekuwa mstari wa mbele katika kuzisaidia nchi za Afrika kwa kutoa msaada wa madawa na madaktari bingwa.

    Mwaka 2006 katika mkutano wa kilele wa ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mjini Beijing,maafisa wa China na Afrika walianzisha hatua za kupanua ushirikiano kati yao,ikiwa ni pamoja na matibabu na afya ya umma.

    China ilitumia takriban $35milioni katika miradi ya afya mwaka 2006.Kufikia mwaka 2014 China ilikuwa ikitoa $150m kila mwaka.

    Serikali ya China inajenga vituo vya afya,inatoa msaada wa vifaa vya matibabu,inatoa fedha pamoja na madaktari.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako