• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • China yakabidhi rasmi hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa serikali ya Kenya

  (GMT+08:00) 2019-05-27 07:35:11

  Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti, ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ilikabidhiwa rasmi kwa serikali ya Kenya mnamo ijumaa tarehe 25 Mei.

  Hospitali hiyo ilijengwa kwa ufadhili wa serikali ya China wa $104mn.

  Mwandishi wetu Khamis Darwesh alihudhuria sherehe hiyo na kutuandalia ripoti ifuatayo.

  Akizungumza katika hafla ya kukabidhi rasmi hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa serikali ya Kenya,Mshauri wa Kiuchumi na Biashara katika Ubalozi wa China nchini Kenya Bw Guo Ce,alisema hospitali hiyo ndio mradi wa kwanza ambao umefadhiliwa na China kupitia mkopo wa masharti nafuu.

  "Huu ni mradi wa kwanza wa ujenzi wa hospitali ambao umefadhiliwa na mkopo wa masharti nafuu wa China wa $104mn.Hospitali hii ina vifaa vya kimataifa vya afya ambavyo ni nadra sana kupatikana sio tu Kenya hata pia China".

  Hospitali hii imejengwa na kampuni ya China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Company Limited.

  Guo alisema kama rafiki na mshirika wa kutegemewa wa maendeleo,serikali ya China inashirikiana kwa ukaribu na serikali ya Kenya na imetoa misaada mikubwa ya kifedha na kiufundi tangu miaka ya 60 kwa nchi ya Kenya.

  "Leo nina furaha sana kwamba mradi huu umekamilika na kukabidhiwa kwa serikali ya Kenya.Ni matumainiyangu kwamba hospitali hii itafunguliwa hivi karibuni na kutoa huduma za afya za kimataifa sio tu kwa wakenya pekee hata pia na watu wengine barani Afrika"

  Mwenyekiti wa Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta Profesa Olive Mugenda alisema kuwa hospitali hiyo itaboresha maisha ya wakenya wengi ambao huenda nchi za nje kutafuta matibabu.

  "Hospitali hii ilianzishwa ili kutoa matibabu ya hali ya juu kwa wagonjwa kutoka Kenya na katika ukanda wa Afrika Mashariki ili iweze kupunguza idadi ya wakenya wanaotafuta matibabu nje ya nchi na kuongeza idadi ya watu kutoka mataifa mengine wanaokuja kutafuta matibabu hapa.Mkakati huu unalenga kupunguzia wakenya gharama za kutafuta matibabu nje ya nchi na pia kuongeza mapato ya serikali"

  Kulingana na Profesa Mugenda ni kuwa miundombinu yote inayohitajika katika hospitali hiyo imekamilika na wataanza kuajiri wafanyakazi mwezi Juni na hatimaye hospitali kufunguliwa rasmi katikati ya mwezi Agosti.

  "Mwisho wa mwezi Julai tutafanya majaribio bila wagonjwa kuhakikisha kwamba vifaa vyote vinafanya kazi ipasavyo halafu mwanzoni mwa mwezi Agosti tutafanya majaribio na wagonjwa na kuhakikisha kwamba mifumo yote inafanya kazi,na tutafungua rasmi hospitali katikati ya mwezi Agosti"

  Aidha hospitali hii inatarajiwa kuwa na kituo cha kwanza kabisa nchini Kenya cha kushughulikia matibabu ya saratani ya matiti.

  Mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua,katika hotuba yake iliyosomwa na mwakilishi wake Kennedy Kihara,alisema kuwa hospitali hii ya kisasa itasaidia Kenya katika kufikia malengo yake ya huduma za afya kwa watu wote.

  "Natoa hakikisho kwamba hospitali hii ina vifaa na teknolojia ya kimataifa.Tuna mashini za kisasa za kugundua na kutibu magonjwa mbalimbali.Mashini ambazo zinapatikana sehemu yoyote katika nchi zilizoendelea.Jambo kubwa ambalo limekuwa likiathiri ubadilishanaji wa fedha za kigeni ni wakenya wanaofanya utalii wa matibabu kwenda kutafuta matibabu katika nchi za nje,kwa hivyo hospitali hii sasa inatarajiwa kubadilisha mwenendo huo.Wale watu ambao walikuwa wakisafiri sehemu mbalimbali za dunia sasa wanaweza kuja hapa na kupata kile ambacho walikuwa nakifuata katika nchi hizo"

  Kwa upande wake,mkandarasi Mkuu kutoka China William Zhong alielezea furaha yake kwa kukabidhi rasmi hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa serikali ya Kenya.

  "Mradi wa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta umefadhiliwa na serikali ya China kupitia mkopo wa masharti nafuu,na kutekelezwa na kampuni ya China Jiangxi .Hospitali hii ina vifaa vya kisasa ambavyo viko tayari kwa ajili ya kutoa huduma kwa watu wa Kenya.Kama mkandarasi,naona faraja kukamilisha kazi hii,na nina hakika itatoa huduma bora za afya Kenya.Nina matumaini kwamba chini ya uongozi wa bodi ya wakurugenzi na juhudi za wafanyakazi,hospitali hii itafunguliwa karibuni na itaboresha viwango vya huduma za afya nchini Kenya"

  Hospitali hii ina vitanda 650 vya wagonjwa,imejengwa katika ardhi ya ekari 100,ina vifaa vya kisasa,ina mashine za kutibu ugonjwa wa saratani,moy na mgongo,ina vitanda 21 katika vyumba vya wagonjwa mahututi,ina eneo la kisasa la watoto waliozaliwa.

  Ujenzi wa hospitali hii ulianza mwaka 2012 na itafunguliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta mwezi Agosti mwaka huu.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako