• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Maonesho ya kwanza ya uchumi na biashara ya China na Afrika yafunguliwa

  (GMT+08:00) 2019-06-27 18:10:57

  Maonesho ya kwanza ya uchumi na biashara ya China na Afrika yamefunguliwa leo mjini Changsha, China. Maonesho hayo yenye kauli mbiu ya "ushirikiano kuleta mafanikio ya pamoja, kuhimiza uhusiano wa uchumi na biashara kati ya China na Afrika", yatahusisha shughuli mbalimbali za biashara, uwekezaji, teknolojia za kilimo, nishati, maeneo ya ushirikiano ya viwanda, miundombinu na ushirikiano wa mitaji.

  Maonesho hayo yameshirikisha China, nchi 53 za Afrika na mashirika kadhaa ya kimataifa, yakiwemo Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa, Shirika la Biashara Duniani na Umoja wa Afrika. Akihutubia kwenye ufunguzi wa maonyesho hayo, Naibu waziri wa biashara wa China Bw. Qian Keming amesema, China inachukulia Afrika kama mwenzi wa dhati katika mchakato wa maendeleo na mambo ya kimataifa. Anasema,

  "Katika miezi minne ya kwanza ya mwaka huu, thamani ya biashara kati ya China na Afrika ilifikia dola bilioni 66 za kimarekani, ambalo ni ongezeko la asilimia 4 ikilinganishwa na mwaka jana wakati kama huu, na wakati huohuo, uwekezaji wa China barani Afrika ulifikia dola bilioni 1.2, ambalo ni ongezeko la asilimia 41."

  Mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka jana mjini Beijing uliamua sekta muhimu za ushirikiano, na kutoa hatua nane kubwa, ambazo kati yao, kuanzisha maonesho ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika ni hatua ya kwanza. Rais Yoweri Museveni wa Uganda akihutubia ufunguzi wa maonesho hayo alisema,

  "China na Afrika zina maoni ya pamoja kuhusu ustawi wa watu wao. Kwa kauli moja zinaona kuwa kuhimiza maendeleo ya viwanda na biashara huria kutakuza uchumi, na kuleta manufaa kwa pande zote. Hivyo tunaweza kusema sasa ni wakati mzuri kuanzisha maonesho hayo."

  Naibu mkurugenzi wa Shirika la Biashara Duniani Bw. Yonov Frederick Agah amesema, kuendeleza ushirikiano ni sehemu muhimu ya uhusiano wa wenzi wa kimkakati kwa pande zote kati ya China na Afrika. Kwa kusaidia ujenzi wa miundombinu, teknolojia ya juu na nafasi za ajira, China imeleta fursa ya maendeleo kwa Afrika. Anasema,

  "Naamini kuwa maonesho ya uchumi na biashara ya China na Afrika yatawatambulisha watu kazi muhimu ya uhusiano wa kunufaishana wa kibiashara katika kuinua kiwango cha kuaminiana katika biashara ya kimataifa."

  Maonesho hayo ya siku tatu yana maeneo matano ya kuonesha matokeo ya ushirikiano kati ya China na Afrika, bidhaa za nchi za Afrika, bidhaa za China, mipango ya ushirikiano, na makampuni ya pande hizo mbili. Maonesho hayo pia yanaweza kuonekana katika tovuti maalumu ya mtandao wa Internet.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako