• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • SOKA: Twenzetu AFCON 2019: Uganda yaonja chungu ya kufungwa yapeta 16 bora, Madagascar yaipiga Nigeria na kufuzu 16 bora

  (GMT+08:00) 2019-07-01 08:44:51

  Madagascar imeshtua baada ya kuichapa Nigeria 2-0 katika mchezo wa mwisho wa Kundi B fainali za kombe la mataifa ya Afrika (AFCON 2019) jana Jumapili uwanja wa Alexandria nchini Misri.

  Ushindi huo umetokana na mabao ya nyota wake, kiungo wa Paris ya Ligue 2 Ufaransa, Lalaina Nomenjanahary dakika ya 13 na mshambuliaji wa Ohod ya Saudi Arabia, Charles Carolus Andriamatsinoro dakika ya 53.

  Kwa matokeo hayo, Madagascar imemaliza kileleni mwa Kundi B ikifikisha pointi saba kufuatia kushinda mechi mbili sare moja, ikifuatiwa na Nigeria iliyomaliza na pointi sita na zote zinasonga hatua ya 16 Bora.

  Guinea pamoja na kuifunga Burundi 2-0, mabao ya mshambuliaji wa Auxerre ya ya Ligue 2 Ufaransa, Mohamed Lamine Yattara dakika za 25 na 52 Uwanja wa Al Salam mjini Cairo, lakini imemaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake nne. Burundi imeshika mkia baada ya kufungwa mechi zote tatu.

  Nayo Uganda imefanikiwa kwenda hatua ya 16 Bora licha ya kuchapwa mabao 2-0 na wenyeji, Misri mabao ya mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah dakika ya 36 na kiungo wa Aston Villa, Ahmed El Mohamady dakika ya 45 na ushei katika mchezo wa Kundi A Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.

  Uganda wamebebwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliyoichapa Zimbabwe 4-0, mabao ya mshambuliaji wa Antwerp ya Ubelgiji, Jonathan Bolingi dakika ya nne, mshambuliaji wa Beijing Guoan ya China, Cedric Bakambu dakika ya 34 na 65 na mshambuliaji wa Middlesbrough ya England, Britt Assombalonga dakika ya 78 Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo.

  Michuano hiyo itaendelea leo kwa mechi za kundi D, Afrika Kusini itakutana na Morocco, huku Namibia itavaana na Ivory Coast huku Kundi C, Kenya na Senegal na Tanzania na Algeria.

  Kwa sasa Algeria inaongoza kundi C kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Kenya yenye pointi tatu sawa na Senegal, wakati Tanzania inashika mkia haina pointi.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako