Katika michuano ya hatua ya robo fainali iliyopigwa jana William Troost-Ekong alifunga goli la aina yake katika dakika za lala salama na kuipaisha Nigeria hadi kwenye nusu fainali za Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika huku Afrika Kusini ikitoka kiwanjani kijasho chembamba kikiwatoka kwa huzuni. Wa kwanza kabisa kuliona lango la Afrika Kusini alikuwa Samuel Chukwueze baada ya kupokea krosi safi kutoka kwa Alex Iwobi na kuwatandika bila huruma Afrika Kusini katika dakika ya 27. Hata hivyo Bongani Zungu alisawazisha kwa mpira wa kichwa uliodaiwa kuwa ameotea kabla ya mfumo unaomsaidia refa wa Video VAR kusema mpira huo ulikuwa umemgonga mchezaji wa Nigeria kabla ya kumfikia. Nigeria itaoneshana ubabe na aidha Ivory Coast au Algeria katika mechi ya pili ya nusu fainali itakayopigwa Jumapili saa mbili usiku.
Nayo Senegal imeingia nusu fainali ya michuano hiyo baada ya goli la kiungo wa kati wa Everton Idrissa Gueye kuwamaliza Benin kwa ushindi mwembamba wa goli moja kwa mtungi. Katika mpambano huo Olivier Verdon wa Benin alilimwa kadi nyekundu na kutolewa nje karibu na mwisho kwa kumfanyia makosa Gueye. Vijana hao wa Aliou Cisse watamenyana na aidha Madagascar au Tunisia kwenye nusu fainali siku ya Jumapili mjini Cairo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |