Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema, wahudumu wa afya wanaandaa kampeni ya chanjo ya surua, ikilenga watoto elfu 67 katika mkoa wa Ituri ulioko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, ambao umekumbwa na mapigano ya kutumia silaha, na pia ni mkoa wa pili ulioathiriwa zaidi na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
Shirika hilo limesema, tangu mwanzo mwa mwaka huu, vifo 1,981 vimeripotiwa nchini DRC kutokana na ugonjwa wa surua, huku theluthi tatu ikiwa ni watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano. Vilevile Shirika hilo limesema, kuanzia mwezi Juni, kesi zaidi ya laki moja za watu wanaoshukiwa kuwa na surua zimeripotiwa, ikiwa ni kiasi kikubwa zaidi ya kile cha mwaka jana.
Maeneo yanayolengwa kupatiwa kwanza chanjo ya surua ni kambi nne za wakimbizi wa ndani zilizoko Bunia, ambazo zimepokea familia nyingi zinazokimbia mapigano katika wiki za karibuni.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |