• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Rais Magufuli wa Tanzania aagiza uchunguzi matumizi ya fedha TAZARA

    (GMT+08:00) 2019-07-27 17:23:16
    RAIS wa Tanzania Dkt. John Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ya nchi hiyo kuchunguza matumizi ya Shilingi Bilioni 15.3 za Tanzania zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kugharamia matumizi ya Mamlaka ya Usafiri wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

    Reli ya TAZARA inayomilikiwa kwa pamoja kati ya serikali ya Tanzania na Zambia ilijengwa kwa ufadhili wa serikali ya Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1975 na ina urefu wa Kilomita 1,860.

    Rais Magufuli alitoa agizo hili Ijumaa, Julai 26, 2019, wakati akizungumza na wafanyakazi na abiria katika kituo cha TAZARA jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuwasili kwa treni ya shirika hilo kutoka mkoani Pwani, wilaya ya Rufiji, ambako aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme.

    Fedha hizo ambazo Rais Magufuli ameagiza zichunguzwe, zilitolewa na serikali ya nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 na 2018/2019.

    Bajeti hiyo ilitengwa kwa ajili ya matengezo ya injini 7 ambazo zingeweza kumudu kusafirisha tani 400,000 za mizigo, kugharamia ukarabati mkubwa wa mitambo mipya ya mgodi wa kokoto za ujenzi wa reli pamoja kuboresha miundombinu ya reli katika stesheni ya Fuga, mkoani Pwani.

    Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema kuwa pamoja na maagizo hayo, Dkt. Magufuli alisema kuwa serikali haiwezi kuiacha TAZARA ife na kwamba atazungumza na Rais wa Zambia Edgar Lungu ili kwa pamoja wachukue hatua madhubuti za kuimarisha miundombinu na kununua injini na mabehewa.

    "Nimesafiri na treni ya TAZARA nimejionea mwenyewe, nataka niwahakikishie sasa nitaelekeza nguvu zangu TAZARA," alisema Rais Magufuli.

    Kwa sasa, TAZARA ambayo reli yake ina uwezo wa kusafirisha tani milioni 5 kwa mwaka inahitaji injini 15 za treni ya mizigo, injini 4 za treni ya abiria na mabehewa 700 ili iweze usafirisha angalau tani 600,000 za mizigo kwa mwaka zitakazozalisha faida, ikilinganishwa na hali ilivyo sasa ambapo inasafirisha tani 250,000 tu kwa mwaka.

    Ili kufanya shirika hilo liweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, tayari uongozi wa TAZARA umeshawasilisha mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ili kuwezesha kila nchi (Tanzania na Zambia) kuwekeza kwa lengo la kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako