• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Rais Magufuli ahaidi kuboresha utendaji kazi wa Reli ya kihistoria Ushirikiano Afrika na China ya TAZARA

    (GMT+08:00) 2019-07-27 17:28:09

    RAIS John Magufuli amesema Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) halitakufa kwa sababu wazo la shirika hilo ni la kihistoria baina ya nchi husika.

    Reli hiyo ya kihistoria ya ushirikiano baina ya nchi za Afrika na China ilijengwa kwa msaada kutoka China, ilianza kutoa huduma mwaka 1975 na kusaidia katika ukombozi wa nchi mbalimbali za Afrika hivyo kupewa jina la Reli ya Uhuru.

    Katika kudumisha ushirikiano hivi karibuni serikali ya China ilionesha nia ya kushiriki katika kukarabati reli hiyo kwa lengo la kuongeza ufanishi kama ilivyokuwa awali.

    Reli ya TAZARA yenye urefu wa kilometa 1,860 ina uwezo wa kusafirisha tani Milioni 5 za mizigo kwa mwaka lakini kutokana na uwekezaji mdogo uliosababisha upungufu mkubwa wa injini na mabehewa inasafirisha chini ya tani laki 3 kwa mwaka.

    Rais Magufuli akiwa katika Stesheni ya TAZARA jijini Dar es Salaam alipokuwa akianza safari ya treni hiyo kutoka Dar es Salaam kuelekea Kisaki Mkoani Morogoro na baadaye Rufiji Mkoani Pwani ambako alikuwa Mgeni Rasmi katika sherehe ya kuweka jiwe la msingi mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji.

    TAZARA inamilikiwa kwa ubia wa asilimia 50 kwa 50 wa nchi ya Tanzania na Zambia hivyo Rais Magufuli anasema shirika hilo halitakufa kwa sababu ni wazo la Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na wa Zambia Pius Kaunda kwa lengo la usafirishaji mizigo.

    Akizungumza na viongozi wa TAZARA amewataka kuwasilisha mapendekezo yao juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuboresha usafirishaji wa mizigo na abiria kupitia TAZARA.

    "Kwahiyo 'it will never die' serikali inatambua umuhimu wa TAZARA na haiwezi kuiacha ikafa au ikifanya kazi kwa ufanisi mdogo usiowaleta manufaa Watanzania kama ilivyokusudiwa," anasema.

    Aliitaka pia menejimenti ya shirika hilo kuzungumza na wafanyakazi na kutatua shida zao na zile ambazo zitashindikana zipelekwe serikalini.

    " wafanyakazi inaonekana wako 'frustrated' nawauliza maswali hawajibu, hawakutaka kuzungumza kwasababu wanaogopa, sio kwamba hawana shida, wanashida kibao inaonekana mnawatisha mtu akizungumza anafukuzwa,"

    Aidha, Rais Magufuli aliagiza mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria kuzifanya nchi zote ziwekeze katika Shirika hilo uharakishwe ili juhudi za kununua injini na mabehewa zifanyike haraka.

    Mkurugenzi Mkuu wa TAZARA, Bruno Chingandu na Meneja Mkuu wa TAZARA Tanzania, Fuad Abdallah walimueleza Rais Magufuli kuwa tayari mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yamewasilishwa Serikalini ili kuwezesha kila nchi kuwekeza katika TAZARA kwa lengo la kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako