• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Juhudi za China katika kutokomeza umaskini uliokithiri zaonyesha mafanikio

    (GMT+08:00) 2019-08-21 13:30:03

    Tangu sera ya mageuzi na kufungua mlango ilipoanza kutekelezwa mwishoni mwa mwaka 1978, China imepata mafanikio makubwa katika kupunguza umaskini. Kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa vya kupunguza umaskini, idadi ya watu wa China wanaokumbwa na umaskini imepungua kwa kiasi kikubwa.

    Takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa, mwaka 1981, asilimia 84 ya watu wa China waliishi chini ya mstari wa kimataifa wa umaskini wa matumizi ya dola 1.25 kwa siku. Hata hivyo, hadi kufikia mwaka 2018, wachumi walitangaza kuwa China iliwakomboa watu milioni 700 kutoka kwenye umaskini.

    Ikiwa nchi kubwa zaidi inayoendelea duniani, China kwa sasa imeshuhudia mabadiliko yaliyoletwa na jitihada za kuondoa mamilioni ya raia wake kutoka kwenye umaskini.

    Mipango ya China ya kupunguza umaskini, imefanikisha ndoto ya kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yaliyokuwa na umaskini, imepunguza pengo la maendeleo kati ya mikoa mbalimbali, na kuboresha uzalishaji na hali ya maisha ya watu maskini.

    Ama kwa hakika, suala la kuwatoa watu katika umaskini limekuwa jambo linalopewa kipaumbele kwa mfululizo tangu mageuzi yalipoanza kuongozwa na kiongozi mkuu wa zamani wa China Deng Xiaoping.

    Rais wa sasa wa China Xi Jinping, ameweka mwaka 2020 kama mwaka ambao nchi yake inatarajia kutokomeza umaskini na kujenga jamii yenye maisha bora kwa pande zote ijulikanayo kwa lugha ya kichina kama "Xiaokang" maana yake ni maisha bora ya kiwango cha kati.

    "Hakuna yeyote atakayeachwa nyuma katika safari ya kuelekea 'Xiaokang'" Rais Xi amekuwa akisisitiza.

    Ndoto hii imenakiliwa vizuri katika kitabu chake kiitwacho "Kuondoa Umaskini" ambapo anasema kwa vyovyote vile "lazima tutokomeze umaskini unaopatikana katika akili zetu kabla ya kuuondoa katika mikoa tunayoongoza, kabla ya kusaidia watu na taifa kujikomboa kutoka kwenye umaskini na kurejea kwenye njia ya ustawi."

    Ni rahisi kuona kwa nini hili lilibaki kuwa lengo kuu. Kwa miaka mingi, China ilikabiliwa na umaskini uliokithiri kutokana na historia, asili yake na hali ya kijamii. Umaskini uliokuwepo ulitajwa kuwa kizingiti kikubwa katika nia ya China ya kujenga jamii yenye maisha bora.

    Watu maskini hawakuishi tu kwenye umaskini kutokana na kipato cha chini, bali walikuwa wanakabiliwa na matatizo kama vile kupata maji, barabara, umeme, elimu, matibabu na mikopo.

    Jamii maskini iliishi katika vijiji vilivyokumbwa na hali ngumu ya maisha, kwenye maeneo yaliyokumbwa na majanga ya asili na sehemu zilizokuwa na miundombinu duni. Kiasi cha uwekezaji na msaada kutoka serikalini hakikuweza kutatua tatizo la kimsingi.

    Baada ya muda, serikali ya China ilifanya utafiti kuhusu sera za kupunguza umaskini kwa kuzingatia viwango anuwai, kutoka kwa watu maskini pamoja na vijiji, wilaya na mikoa iliyozongwa na ufukara.

    Juhudi zilizoongozwa na serikali za kuondoa umaskini zikageuzwa kutoka misaada ya kiuchumi katika miaka ya 70 na 80, na kuanza kuzingatia kuboresha uwezo wa watu maskini kujiendeleza ili kuondoa umaskini na kuwezesha vijiji na jamii zao kupata maendeleo.

    Mwaka 1986, kwa mfano, serikali ya China ilianzisha taasisi maalum kwa ajili ya kupambana na umaskini. Ilipoanza kutekeleza mipango mahususi ya kupunguza kiwango cha umaskini, vita dhidi ya umaskini nchini China iliingia zama mpya.

    Muda mfupi baadaye lengo likabadilika kutoka kupunguza umaskini kupitia msaada hadi kupunguza umaskini kwa njia ya kujiendeleza. Moja kwa moja China ikaanza kuchunguza miradi ya kusaidia kupunguza umaskini kimaendeleo.

    Mbinu hii ililenga kutumia maliasili katika maeneo maskini kuongeza uzalishaji na serikali kutoa msaada kwa familia maskini.

    Watu katika maeneo haya walipozidi kujiendeleza na kujifunza jinsi ya kuongeza uzalishaji, waliweza kujitoa katika umaskini wao wenyewe. Kujiendeleza kwa kupunguza umaskini pia kulihusisha hatua nyingine mbalimbali kama vile kuboresha miundombinu, kukuza maendeleo ya elimu na huduma za afya pamoja na utoaji wa sera za mikopo zenye upendeleo kwa wenyeji.

    Eneo la Xiangxi kwenye Jimbo la Hunan, kwa mfano, lilikuwa sehemu maskini zaidi ambapo watu zaidi ya milioni 1.5 waliishi chini ya mstari wa umaskini katika miaka ya 80. Asilimia 84 walikuwa wakiishi maisha ya dhiki, na kuondokana na umaskini kulikuwa ndoto ya kila mtu aliyeishi katika eneo hilo.

    Marekebisho yaliyotekelezwa kwa utaratibu maalum, yaliwezesha kupunguzwa kwa hali ya umaskini kwa kuongeza tija na kuboresha miundombinu ya msingi katika maeneo ya vijijini. Hii ilifanyika kupitia kwa mfumo wa kuleta mageuzi kwa bei ya mazao ya kilimo, na maendeleo ya miji na vijiji.

    Tangu mwaka 2000, vijiji vya mbali vilivyokuwa na umaskini zaidi vililengwa kwa ajili ya kupunguza umaskini. Wakati huu, mkakati ulihusisha maendeleo ya viwanda, miundombinu, ikolojia na mafunzo ya kazi.

    Miradi mikubwa ya viwanda ilipewa kipaumbele katika maeneo ya vijijini. Kwa ujumla, hii ilisababisha maendeleo ya viwanda ikiwa ni pamoja na kilimo cha kiwango kikubwa cha matunda ya kiwi, chai, maua, tumbaku na mitishamba ya tiba ya jadi ya Kichina iliyochukua maelfu ya hekari.

    Historia ya kupunguza umaskini katika eneo la Xiangxi ya zaidi ya miaka 30 ni mfano wa jinsi China ilivyopigana na janga la umaskini kwa ujumla.

    "China ni nchi ya kwanza kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Maendeleo yake, hasa katika suala la kupunguza umaskini, ni mchango mkubwa kwa ulimwengu." Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alisema.

    Baada ya miongo ya majaribu na matatizo, vita ya kupunguza umaskini nchini China imepata matokeo yanayoleta matumaini. China kamwe haitakoma kujaribu kufikia lengo lake la kuwa na jamii isiyo na umaskini ifikapo mwaka 2020.

    Maelezo ya picha:

    Rais Xi Jinping anazungumza na wenyeji wa kijiji cha Shibadong katika Mji wa Paibi ulioko kaunti ya Huayuan ya eneo linalojiendesha la kabila la Watujia na Wamiao la Xiangxi, Mkoa wa Hunan, China, Novemba 3, mwaka 2013. Picha kwa hisani ya Xinhua

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako