• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Jinsi tetemeko kubwa la ardhi la 2008 lilivyowapelekea Wachina kufanya juhudi za pamoja kwa kujijenga upya

  (GMT+08:00) 2019-08-22 10:24:43

  Mei 12, mwaka 2008, tetemeko kubwa la ardhi lilitokea kwenye Wilaya ya Wenchuan mkoani Sichuan, kusini magharibi mwa China, na kusababisha idadi kubwa ya vifo na majeruhi, pamoja na uharibifu mkubwa wa mali, miundombinu, viwanda, kilimo na huduma za kijamii, katika mikoa ya Sichuan, Gansu na Shaanxi.

  Siku hiyo iliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama wakati mbaya zaidi katika historia ya China. Sehemu hiyo ya nchi ilibaki huku watu 70,000 wakipoteza maisha yao, na mamia ya maelfu ya manusura walibakia na makovu. Mamilioni ya wale walionusurika walijikuta hawana sehemu za kuishi kwa kuwa nyumba zao ziliharibiwa na tetemeko hilo.

  Katika ziara yangu ya Sichuan hivi karibuni, kwa kutembelea mabaki ya makumbusho ya tetemeko hilo, nilishuhudia viwango vya uharibifu kwa miundombinu ikiwemo mifumo ya maji, umeme na gesi na jinsi mifumo ya mawasiliano ya simu na usafiri ilivyovurugika.

  Miundombinu muhimu iliharibiwa vibaya, huku mamia ya shule na vituo vya afya pamoja na maelfu ya kilomita za barabara zikiharibiwa katika eneo ambalo tayari lilikuwa miongoni mwa sehemu maskini nchini China.

  Hili halikuwa tu janga la kibinadamu, bali pia lilikuwa mtihani mkubwa wa kisiasa kwa Chama tawala yaani Chama cha Kikomunisti cha China CPC, na ni mtihani ambao chama hicho kilifaulu kwa matokeo ya kuvutia.

  Mara tu baada ya tetemeko hilo, kazi ngumu ya kujenga upya maeneo yaliyokumbwa na majanga ilianza. Serikali ya China ilikuwa na nia ya kuwarejesha waathirika wa tetemeko hilo maisha yao ya kawaida kwa haraka. Bila kupoteza muda, serikali ilizindua idara maalum ya kuongoza mchakato wa ukarabati hasa kwa vijiji wanavyoishi jamii masikini.

  Serikali kuu ya China jijini Beijing ilituma vikosi vya uokoaji mara moja, vilivyojumuisha wauguzi na maelfu ya wanajeshi katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko.

  Serikali pia ilitangaza ratiba ya operesheni hiyo ya ukarabati. Wale waliopewa nafasi ya kuongoza kazi hii ngumu walibidi kukidhi mahitaji ya kukamilisha kazi ya kujenga upya ndani ya muda mfupi iwezekanavyo.

  Wakati huo huo, serikali iliratibu na kuongoza juhudi za kusaidia mikoa iliyoathirika kwa kukusanya rasilimali kwa ajili ya ukarabati huo hatua kwa hatua kwa mpango na kwa ufanisi.

  Katika kila makao makuu ya ukarabati, katika kila sehemu ya ukarabati, katika kila kijiji au mji wa ukarabati, zilisikika hadithi za kugusa kuhusu watu waliofanya kila wawezalo katika ukarabati wa maeneo yaliyoathirika.

  "Baada ya janga la kiwango kile, Chama tawala pamoja na majeshi yetu na watu kutoka sehemu mbalimbali kote nchini walijitolea na kuunga mkono juhudi za Kamati Kuu ya CPC na Baraza la Mashauriano ya Kisiasa kukabiliana na hali ngumu iliyojiri wakati huo." Mkuu wa Wilaya ya Lixian, Wang Shiwei alisema.

  Ingawa jumuiya ya kimataifa iliitikia na kutoa mchango wake kusaidia wahanga wa janga hilo, serikali za mitaa na raia walifanya kazi bega kwa bega kuhakikisha hali ya kawaida inarejea.

  Ili kufanikisha mchakato huu, serikali iliamuru mikoa tajiri kwenye sehemu ya mashariki na ya kati kutoa asilimia fulani ya rasilimali zao kwa kila wilaya iliyokumbwa na tetemeko mkoani Sichuan.

  Mwishoni mwa mwaka 2009, ujenzi wa nyumba vijijini ulikamilika katika Wilaya ya Wenchuan na kuruhusu ujenzi wa vituo vya huduma kwa umma kuendelea.

  Matokeo ya awali ya ujenzi huu yalikuwa mafanikio katika ujenzi wa viwanda na marekebisho ya kimsingi mijini. Huduma za soko zikarejeshwa, pamoja na mfumo wa mazingira ya asili, bila kusahau matumizi bora ya ardhi.

  Kiwango cha uratibu kilichotumika kupambana na janga kubwa kiasi kile kilikuwa cha kipekee.

  Mafanikio yaliyoandikishwa katika ukarabati wa sehemu iliyoathirika na tetemeko la ardhi la Wenchuan, yanaenda sambamba na mafanikio ya msaada wa kimaendeleo unaofuatwa na serikali ya China.

  Muda ambao serikali ya China ilitumia kurejesha hali ya kawaida katika sehemu iliyokumbwa na tetemeko hilo umesifiwa sana.

  Swala lililofuatiliwa zaidi ni kasi ambayo serikali ya China iliyotumia kuhamasisha mashirika ya serikali, sekta binafsi na raia wake kwa jumla kufanikisha juhudi hizo.

  Kitu kingine cha kuvutia katika ukarabati huo kilikuwa jinsi serikali za mitaa zilivyoshiriki kwenye mchakato huo. Serikali kuu ilioanisha kila wilaya iliyoathirika na mkoa ambao haukuathiriwa. Hii ilitoa fursa ya ushirikiano kati ya mikoa, hatua ambayo ilisaidia kuhamasisha msaada wa kifedha na kiufundi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati.

  Miaka mitatu baada ya tetemeko la ardhi la Wenchuan, China ilijenga shule takriban 3,000 na vituo vya afya zaidi ya 1,000 ili kutoa huduma bora kwa umma. Mpango wa ustawi pia ulipanuliwa ili kuwasaidia watu milioni 1.4 waliokumbwa na hali duni kimaisha kutokana na tetemeko hilo.

  Ujenzi huo haukusimama na umekuwa ukiendelea kwa miaka 11 iliyopita. Hali ya maisha ya watu imekuwa bora na uchumi kuimarika. Mamia ya maeneo ya makazi mapya yalijengwa na maelfu ya familia kuhamia katika nyumba mpya.

  Kanuni ya kimsingi ya serikali ya China ya "raia kwanza" iliwezesha familia maskini kufuatiliwa kwa njia maalum.

  Uzoefu mkubwa wa China na utaalamu wake wa kupambana na majanga na kutoa misaada katika miaka 11 iliyopita unatoa somo muhimu kwa nchi nyingine juu ya umuhimu wa mshikamano wakati wa majanga.

  Maelezo ya picha

  Magofu ya shule ya Xuankou katika mji wa Yingxiu, ambayo kwa sasa ni sehemu ya kumbukumbu ya tetemeko la ardhi mkoani Sichuan China tarehe 12 Mei, 2008. / Picha kwa hisani ya CGTN

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako