• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Nilivyomfahamu Robet Mugabe

  (GMT+08:00) 2019-09-06 19:17:12

                                                                                           Hii ni picha ya Bw. Liu Kegong na Bw. Robert Mugabe alipotembelea mradi unaojengwa na kampuni ya China

  Rais 6 alasiri, rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe kwenye account yake ya mtandao wa kijamii ametoa taarifa akitangaza kuwa, rais wa zamani wa nchi hiyo Bw. Robert Mugabe amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.

  Bw. Mugabe ni kiongozi na mwanasiasa hodari wa Zimbabwe ambaye aliwaongoza wazimbabwe kupata ukombozi, kulinda maslahi ya kitaifa, kupinga kuingiliwa na nchi za nje katika mambo ya ndani, na kuhimiza uhusiano kati ya nchi hiyo na China. Tangu Mugabe aingie madarakani mwaka 1980, Zimbabwe imeiunga mkono kithabiti China katika masuala mbalimbali yakiwemo Taiwan, Tibet na haki miliki, na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili umeendelea vizuri katika uchumi, biashara, elimu, utamaduni, sayansi na sekta nyinginezo. Bw. Mugabe aliwahi kusema wazimbabwe hawatasahau msaada wa dhati wa China katika mchakato wa kupigia ukombozi wa Zimbabwe. Yafuatayo ni baadhi ya mambo yaliyotokea kati ya wachina kadhaa na  Bw. Mugabe.

  Mwezi Julai mwaka 1984, mchina Bw. Liu Kegong alifika Zimbabwe kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Harare, ambao unajulikana kama "Mnara Mkuu wa Urafiki kati ya Watu wa China na Zimbabwe". Anasema, 

  "Mimi naitwa Liu Kegong, natoka mkoa wa Fujian, China. Mimi ni fundi mwashi. Mwaka 1984 nilikwenda Zimbabwe kushiriki kwenye ujenzi wa Uwanja wa Michezo ya Harare. Nilifanya kazi nikiwaongoza zaidi ya wafanyakazi wenyeji 30. Ili kuelewana nao vizuri, nilijifunza lugha ya Kishona. Miaka 7 baadaye, nilipewa kazi nyingine nchini Zimbabwe, kwa kuwa najua Kishona."

  Siku moja ya mwaka 1991, Bw. Mugabe alipofanya ziara ya ukaguzi katika mradi wa ujenzi uliotekelezwa na wachina, alimkuta Bw. Liu. Alishangaa sana kuona Bw. Liu anaweza kuongea Kishona, na kumchukulia kama rafiki mkubwa. Baadaye kila Mugabe alipokagua mradi huo, alifanya mazungumzo na Bw. Liu. Bw. Liu anasema,

  "Nakumbuka kuwa rais Mugabe alikuwa mtu mwema sana, alinichukulia kama rafiki, na kuniita 'mwenzangu'"

  Bw. Liu anaona Mugabe ni kiongozi bora ambaye aliwapenda sana wananchi wake, na pia alitoa mchango mkubwa kwa ajili ya kuhimiza urafiki kati ya Zimbabwe na China. Anasema,

  "Nilimtembelea nyumbani kwake. Wakati huo mama yake alikuwa na umri mkubwa, lakini hawakuwa na taa ya umeme. Napenda sana Zimbabwe, na watu wa hapa ni wazuri."

  Bibi Yin Liqing ni mwanahabari wa Radio China Kimataifa. Mwezi Agosti mwaka 1996, alikusanya habari katika harusi ya Bw. Mugabe. Anasema, 

  "Harusi hiyo ilinitambulisha afya nzuri ya Bw. Mugabe. Kwa mzee mwenye umri zaidi ya miaka 70, shughuli mbalimbali za harusi kweli zingemchosha. Lakini hakujali hata kidogo."

  Mke wa zamani wa Bw. Mugabe alifariki dunia mwaka 1991, kutokana na ugonjwa. Wazimbabwe walikuwa wanatumai sana apate mke mpya, hivyo harusi yake ilifuatiliwa sana na watu wote. Bibi Yin amesema harusi hiyo ilifanyika katika kanisa moja dogo nyumbani kwa kina Mugabe, ambalo liliweza kuwapokea watu karibu mia moja tu, lakini zaidi ya wageni mia mbili walikwenda. Bibi Yin anasema, 

  "Wageni walikabidhiana sanduku moja dogo. Hatukujua walikuwa wanafanya nini, mpaka tulipopewa sanduku hilo. Kumbe walikuwa wanachangisha fedha za zawadi, dola kumi au ishirini za kizimbabwe. Tulitoa dola 80 kwani 8 ni namba ya bahati nzuri kufuatia desturi ya kichina. Wageni walipiga makofi kwa kwa wanaona tumetoa pesa nyingi."

  Harusi hiyo ilifanyika kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 7 ya adhuhuri, na wageni wengi walikunywa pombe nyingi kutokana na furaha kubwa. Bw. Xin Shunkang alikuwa balozi wa China nchini Zimbabwe kuanzia mwezi Julai mwaka 2009 hadi mwezi Julai mwaka 2012. Katika miaka hiyo mitatu, kupitia ubalozi wake, China ilitoa misaada mbalimbali kwa Zimbabwe, ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba ya watoto yatima na shule mbili za msingi, kukarabati Uwanja wa Ndege wa Viktoria, kutoa misaada ya chakula wakati wa maafa, kutuma madaktari kuwatibu wagonjwa zaidi ya 900 wa macho, na kuandaa mafunzo nchini China kwa watu zaidi ya 300 ya Zimbabwe. Bw. Mugabe aliishukuru China akisema China pia ni nyumbani kwake. Bw. Xin anasema, 

  "Nakumbuka vizuri hali ya mazungumzo kati ya Bw. Mugabe na Bw. Hu Jintao aliyekuwa rais wa China. Baada ya hotuba ya Rais Hu, Bw. Mugabe alifafanua maoni yake na msimamo wa Zimbabwe. Nilishangaa uwezo wake wa kukumbuka na kujumuisha."

  Bw. Xin pia anakumbuka vizuri hali ilivyokuwa wakati ubalozi wa China unasherehekea siku ya kuzaliwa ya Mugabe miaka 9 iliyopita. Hii ilikuwa mara pekee ya Mugabe aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa katika ubalozi wa nchi za nje. Bw. Xin anasema, 

  "Tulimkaribisha rais Mugabe kwa ukarimu mkubwa katika ubalozi wetu. Jambo lililomshangaza zaidi ni kwamba, wanadiplomasia wetu waliimba wimbo wa taifa wa Zimbabwe kwa lugha ya Kishona."

  Bw. Mugabe aliipenda sana China, hata nyumba yake mjini Harake ina mtindo wa kichina. Upendo wake kwa China unatokana na desturi ya kusaidiana ya nchi hizo mbili, na pia unatokana na kanuni ya kufahamiana na kuheshimiana, na malengo ya pamoja ya kuendeleza uchumi na kuboresha maisha ya watu. Maelezo ya wachina hao kuhusu mambo yaliyotokea kati yao na Bw. Mugabe yameonesha urafiki mkubwa kati ya nchi hizo mbili.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako