Bingwa mara mbili wa mbio za mita 800 kwenye michezo ya Olimpiki, Caster Semenya ameanza kujiandaa kwa maisha mapya nje ya riadha baada ya kujiunga na klabu moja ya soka ya wanawake.
kwa sasa anakata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya kusikiza kesi za michezo (CAS) iliyoidhinisha matumizi ya sheria za Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) zinazotaka wanawake walio na homoni za juu za 'testosterone' kutumia dawa kuzipunguza kabla ya kushiriki mashindano yoyote.
Semenya hawezi kutetea taji lake la dunia la mbio za mita 800 jijini Doha nchini Qatar baadaye mwezi huu bila ya kutumia dawa za kupunguza homoni hizo, kitu ambacho amekataa kufanya.
raia huyo wa Afrika Kusini ameanza kufanya mazoezi na klabu ya JVW FC kutoka mjini Gauteng Afrika Kusini, akinuia kusakata mechi yake ya kwanza msimu ujao kwa sababu wakati huu kipindi cha kusajili wachezaji kimefungwa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |