• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yatarajia kutimiza lengo la maendeleo ya uchumi

    (GMT+08:00) 2019-09-16 18:30:55

    Idara kuu ya takwimu ya China leo imetangaza takwimu ya maendeleo ya sekta muhimu za kiuchumi zikiwemo viwanda, matumizi na uwekezaji katika mwezi wa Agosti. Msemaji wa idara hiyo Bw. Fu Linghui amesema, katika mwezi uliopita, kwa ujumla uchumi wa China umedumisha mwelekeo mzuri wa maendeleo, na China ina msingi, mazingira na imani katika kutimiza lengo lake la kiuchumi kwa mwaka huu.

    Kwenye mkutano na wanahabari uliofanyika leo katika ofisi ya habari ya Baraza la Serikali la China, msemaji wa idara kuu ya takwimu ya China Bw. Fu Linghui ametathmini hali ya maendeleo ya uchumi wa China katika mwezi wa Agosti, akisema,

    "Kwa mwezi Agosti, takwimu kuu za kiuchumi ziko katika hali tofauti. Kasi ya maendeleo ya viwanda ilipungua kidogo, huku sekta ya huduma ikikua kwa haraka zaidi. Wakati huohuo, mauzo ya bidhaa yamedumisha utulivu, na kasi ya ongezeko la uwekezaji ilipungua kidogo. Lakini kwa jumla, ni hali ya kawaida kutokea kwa mabadiliko haya katika mwezi mmoja kutokana na sababu mbalimbali. Tunaona kuwa uchumi wetu umedumisha utulivu."

    Kwa upande wa uzalishaji, katika miezi minane iliyopita ya mwaka huu, thamani ya uzalishaji wa viwanda vikubwa imeongezeka kwa asilimia 5.8 ikilinganishwa na mwaka jana wakati kama huu, na kati yao uzalishaji wa teknolojia ya juu umekua kwa asilimia 8.4.

    Kwa upande wa mahitaji, katika miezi minane iliyopita, thamani ya mauzo ya bidhaa za rejereja imeongezeka kwa asilimia 8.2 ikilinganishwa na mwaka jana wakati kama huu. Bw. Fu anasema,

    "Tukitoa mauzo ya magari, kasi ya ongezeko la mauzo ya bidhaa za rejereja kwa mwezi wa Agosti iliongezeka kwa asilimia 9.3 ikilinganishwa na mwezi Agosti mwaka jana, na kuzidi mwezi Julai kwa asilimia 0.5. Wakati huohuo, matumizi ya huduma yameongezeka kwa kasi."

    Aidha, katika miezi minane iliyopita, uwekezaji wa mali za kudumu umeongezeka kwa asilimia 5.5. Uwekezaji katika uhifadhi wa mazingira, elimu na teknolojia ya juu umeongezeka kwa kasi zaidi.

    Katika miezi minane iliyopita, biashara kati ya China na nchi za nje imeongezeka kwa asilimia 3.6, na mauzo ya bidhaa za China katika nchi za nje yameongezeka kwa asilimia 6.1. Wakati huohuo, matumizi halisi ya uwekezaji wa nje nchini China yameongezeka kwa asilimia 6.9.

    Bw. Fu anaona kuwa, mwaka huu kasi ya ongezeko la biashara ya kimataifa imepungua kutokana na mabadiliko ya mazingira ya kiuchumi, na hivi sasa China iko katika kipindi kigumu cha marekebisho ya muundo wa uchumi, hivyo uchumi wa China unakabiliwa na changamoto mbalimbali, lakini kwa ujumla utadumisha maendeleo yenye utulivu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako