Mkuu wa idara kuu ya posta ya China Bw. Ma Junsheng leo hapa Beijing amesema, katika miaka 70 iliyopita tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, huduma za posta nchini China zimekua kwa mara 7,700, na China imekamilisha kimsingi mtandao wa kisasa wa posta.
Takwimu zinaonesha kuwa thamani ya huduma za posta nchini China kwa mwaka jana ilifikia karibu dola bilioni 170 za kimarekani, na vifurushi vilivyopelekwa viliongezeka na kuzidi bilioni 50 kutoka zaidi ya milioni 1.5 katika miaka ya 80 ya karne iliyopita. Mkuu wa idara kuu ya posta ya China Bw. Ma Junsheng anasema,
"China imekuwa soko la posta lenye uhai zaidi na linaloendelea kwa kasi zaidi duniani. Idadi ya vifurushi vya haraka nchini China imezidi idadi hiyo ya jumla ya nchi zilizoendelea zikiwemo Marekani, Japan na nchi za Umoja wa Ulaya. China imechangia asilimia 50 ya maendeleo ya soko la posta la kimataifa.
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 95 ya vijiji nchini China vimepata huduma za vifurushi vya haraka, na mtandao wa posta wa moja kwa moja kati ya vijiji umekamilika. Mwaka jana idara za posta nchini China zimewahudumia watu kwa mara zaidi ya bilioni 100, na thamani ya biashara kupitia posta imefikia karibu dola trilioni moja za kimarekani. Wakati huohuo, maendeleo ya huduma za posta pia yanaongeza ajira zaidi ya laki mbili kila mwaka.
Aidha, matumizi ya teknolojia ya kisasa katika huduma za posta yameongezeka kidhahiri. Mwaka jana China ilijenga zaidi ya vituo 200 vya kugawanya vifurushi vinavyotumia akili bandia. Mbali na hayo, teknolojia za big data, hesabu ya mawingu (cloud compyuting), na mtandao wa kuunganisha vifaa nyumbani pia zimetumiwa katika huduma za posta. Bw. Ma amesema hatua ijayo ni kuhimiza huduma za vifurushi vya haraka kuingia zaidi vijijini.
Hadi sasa China imeanzisha mawasiliano ya posta na zaidi ya nchi na sehemu 200 duniani. Kutokana na utandawazi wa uchumi, huduma za vifurushi vya haraka za kuvuka mipaka zinaongezeka kwa haraka. Bw. Ma ameeleza kuwa makampuni ya vifurushi vya haraka ya China yataharakisha kujenga mitandao katika nchi muhimu, akisema,
"Kufuatia mahitaji ya makampuni yanayouza bidhaa mtandaoni, tutapiga hatua katika nchi za kusini mashariki mwa Asia, na kupanua soko la Marekani, Ulaya, Japan, Korea ya Kusini, nchi zinazoibuka kiuchumi, na nchi zilizojiunga na 'Ukanda Mmoja, Njia Moja'. Pia tutaunga mkono makampuni ya posta kupanua biashara zao, na kuongeza uwezo wa kuzoea masoko mapya. Aidha, tutaimarisha ushirikiano na makampuni ya kimataifa, ili kujenga mtandao wa kimataifa wa posta wenye usalama, na kuweza kufika sehemu mbalimbali.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |