• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Miaka 70 -- tumeipita kwa kusaidiana na kushirikiana – ripoti maalumu ya kuadhimsha miaka 70 ya Jamhuri ya Watu wa China

    (GMT+08:00) 2019-09-30 09:25:47

    Huu ni mwaka wa 70 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China. Katika miaka 70 iliyopita, China imetekeleza sera ya kidiplomasia ya amani na kujiamulia, na kwa kufuata utaratibu wa kimsingi wa uhusiano wa kimataifa ambao kiini chake ni kanuni tano za kuishi kwa pamoja kwa amani。China imeshirikiana na nchi zinazoendelea kwa msimamo thabiti, ili kujitahidi kujenga utaratibu mpya wa kimataifa ulio wa haki na usawa zaidi, na kuhimiza amani, masikilizano na maendeleo ya dunia. Katika mchakato huo, China imedumisha urafiki mkubwa na nchi za Afrika, ambapo pande hizo mbili zimefanikiwa kujenga uhusiano wa wenzi wa kimkakati katika zama mpya, na zinajitahidi kujenga jumuiya yenye mustakbali wa pamoja, ili kusukuma mbele zaidi uhusiano kati yao. Maendeleo ya uhusiano kati ya China na Afrika ni utendaji wa ujenzi wa pamoja wa China na nchi nyingine wa jumuiya yenye hatma ya pamoja, na pia yameonesha uhai mkubwa wa mawazo ya sera ya kidiplomasia ya China.

    Wakati Jamhuri ya Watu wa China ilipoanzishwa, kizazi cha kwanza cha kiongozi wa China kiliziunga mkono kwa nguvu kubwa nchi za Afrika kujipatia ukombozi na uhuru, na kutoa msaada kwa ajili ya ustawi wa Afrika licha ya kuwa nyuma kimaendeleo. Kwa upande mwingine, nchi za Afrika ziliiunga mkono China kurejesha kiti chake katika Umoja wa Mataifa na haki zake nyingine halali. Zambia ndiyo moja ya nchi za Afrika zilizoisaidia China kurejea kwenye Umoja wa Mataifa. Mwaka 1964, chini ya uongozi wa Bw. Kenneth Kaunda, nchi hiyo ilipata uhuru. Miaka mitatu baadaye, alifanya ziara nchini China, na kufanikiwa kushawishi China kutoa msaada wa kujenga Reli ya TAZARA yenye urefu wa kilomita 1,860.

    Mjumbe wa kwanza wa Zambia katika Umoja wa Mataifa ambaye pia alikuwa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Bw. Vernon Mwaanga aliunga mkono China kurejea kwenye Umoja wa Mataifa, na kutoa hotuba ya pongezi baada ya China kufanikiwa kurejea kwenye umoja huo kwa niaba ya nchi za Afrika mwaka 1971. Baada ya kustaafu, Bw. Mwaanga ameendelea kusukuma mbele uhusiano wa kirafiki kati ya Zambia na China, na kujulisha mara nyingi uzoefu wa maendeleo ya China kwa pande mbalimbali za Zambia. Anasema,

    "Mimi na balozi wa Tanzania Bw. Salim Ahmed Salim sote tuliunga mkono maazimio muhimu ya kurejesha kiti cha China katika Umoja wa Mataifa. Hatimaye, mwaka 1971 tulifanikiwa kuisaidia China kurejea kwenye Umoja wa Mataifa. Huu ni mnara muhimu wa kihistoria, kwani tunaona kuwa umoja huo ni shirika kuu la kimataifa ambalo linapaswa kufuata kanuni ya uwakilishi mkubwa, na haifai kutengana na nchi kubwa yenye watu zaidi ya bilioni 1.3. China ilikuwa mwenzi muhimu wa nchi za Afrika katika kupambana na ukoloni na ubaguzi wa rangi, na tunatumai kujenga dunia yenye haki na utulivu zaidi. Mimi ni mmoja wa kikundi cha mwisho cha wageni waliokutana na aliyekuwa waziri mkuu wa China Zhou Enlai baada ya kulazwa hospitali mwaka 1975. Wakati huo mimi nilikuwa waziri wa mambo ya nje. Bw. Zhou aliposikia nimekuja, alinialika kumtembelea. Niliona fahari kubwa kwamba nchi yetu inaweza kushirikiana na China katika kujiendeleza. China haitasahau nchi za Afrika zilizoisaidia kurejea kwenye Umoja wa Mataifa. Mwaka 1971, kwa niaba ya nchi za Afrika, nilimpongeza balozi wa kwanza wa China katika Umoja wa Mataifa Bw. Huang Hua, na kuikaribisha China kurudi kwenye umoja huo. Natumai nitapata nafasi ya kutembelea China tena, ambayo itakuwa mara yangu ya 20 kuitembelea nchi hiyo."

    Tarehe 14 mwezi Julai mwaka 1976, Reli ya TAZARA iliyojengwa kwa misaada ya China ilizinduliwa rasmi. Huu ulikuwa mradi mkubwa zaidi wa misaada ya China tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China. Aliyekuwa rais wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere alisema, kuzinduliwa kwa reli hiyo ni kama kulipua bomu la nyuklia. Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860 inapita kwenye maeneo mengi yasiyo na watu. Bw. Xu Jilin mwenye umri wa miaka 90 alishiriki mara tatu kwenye ujenzi wa reli hiyo, na kufanya kazi nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 6. Anasema,

    "Tulipofanya kazi kulikuwa sehemu isiyo na wakazi. Wajenzi wa kienyeji walikwenda pamoja na familia yao. Hatukuwa na makazi rasmi, hivyo tulishirikiana kujenga nyumba kwa nyasi. Kutokana na upungufu wa maji ya kunywa, tulikwenda mbali kwa gari ili kuchota maji. Wajenzi wenyeji pia hawakuwa na maji ya kunywa, na wanawake na watoto wao walitembea umbali mrefu ili kupata maji. Baada ya kujua hali hii, tulituma magari yetu kuwasaidia kuchota maji. Kwenye jiko letu, kulikuwa na wapishi watatu tu. Marafiki zetu wenyeji walijitolea kutusaidia. Wakati tulipohitaji kuni, walikwenda msituni kuzikusanya kwa ajili yetu. Tuliishi pamoja kwa kushirikiana na kusaidiana. Tulipoagana, walisema wachina, marafiki, kwa herini. Natumai China na Afrika zitadumisha urafiki daima."

    Reli hiyo inayosifiwa kama reli ya uhuru ya Afrika ni daraja la urafiki kati ya China na Afrika, na pia ni mnara mkubwa wa kumbukumbu ya urafiki huo. Hadi sasa kwenye vituo vya reli hiyo nchini Tanzania, kuna picha za waliokuwa viongozi wa China, Tanzania na Zambia wakati wa ujenzi wa reli hiyo. Bw. Fares Mgona ni mfanyakazi mstaafu wa maktaba ya taifa ya Tanzania, na hadi sasa anakumbuka maneno ya Mwenyekiti Mao Zedong aliyekuwa kiongozi wa China wakati ule. Anasema, 

    "Kwenye upande wa uhusiano wa Tanzania na China ni kweli ulianza zamani, hasa kipindi cha rais wetu wa kwanza mwalimu Julius Nyerere kulikuwa na uhusiano mzuri kati ya China na Tanzania hasa pale Mao Zedong ambaye alikuwa mwenyekiti wa chama kikomunisti tunaweza kumwita mwanamapinduzi kwa sababu ndiye aliwezesha kuleta mapinduzi kati ya Tanzania na China, tukikumbuka zaidi kwenye suala la reli ya TAZARA kati ya Tanzania na Zambia kipindi cha miaka 1980. Kwa hivyo ukimwangalia Mwenyekiti Mao mtu aliyeanzisha mahusiano yetu na China, na ukiangalia mahusiano bado yapo. Kutoka kipindi kile cha utawala wa Nyerere uhusiano umeweza kuendelea kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo, kama vile uchumi na miundombinu. Ukiangalia katika historia kuna viwanda ambavyo viliwekezwa na wachina, kwa mfano kiwanda cha nguo cha urafiki ambacho kinafanya kazi hadi leo hii. Mwalimu Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong walikuwa na mahusiano maalum, hasa aliposema uhusiano wa Tanzania na China umekua zaidi, na kumshukuru kwa maendeleo aliyoleta nchini Tanzania baada ya serikali yake kufadhili ujenzi wa Reli yenye urefu wa kilomita 1,860 kutoka Tanzania –Zambia (TAZARA) iliyojengwa na wachina kwenye miaka ya sabini. Mwalimu Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong walikuwa na mambo mengi yanayofanana. Mwalimu Nyerere alikuwa mwanzilishi wa Taifa sawa na mwenyekiti Mao Zedong kwa China. Mwenyekiti Mao alipenda sana kutumia nukuu alipokuwa anataka kueleza jambo na hizi ni baadhi ya nukuu alipenda sana kutumia na mimi kama mtu niliweza kufikia historia hii nilizipenda sana ni: 'Umuamshapo chui tumia fimbo ndefu' katika nukuu zake alizozitoa zilikuwa zinaleta tafsiri nyingi hasa za kimahusiano na za kiuchumi kwa hivyo nukuu zake zimekuwa chachu katika kutukumbusha mambo Fulani ya urafiki wetu. 'Mabadiliko yoyote sio sherehe ya chakula cha jioni, au sio uandishi wa insha, au sio uchoraji wa picha au sio ushonaji.' 'Mtu hawezi kuendelea bila makosa ni lazima makosa yawepo.' 'Siasa ni vita bila umwangaji damu, wakati vita ni siasa na umwagaji damu'."

    Tangu China ianze kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, imerekebisha njia yake ya kusaidia Afrika ili iwe endelevu. Ofisa wa habari wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Nairobi Bw. Cavince Adhere amesema, mchakato wa China wa kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango pia ni mchakato wa makampuni ya China kutoka nje na kufika sehemu nyingine duniani. Ameongeza kuwa Afrika ni sehemu muhimu ya China kutekeleza sera ya kufungua mlango, na makampuni mengi ya China yakiwemo Huawei, Luqiao yamestawisha shughuli zao barani Afrika, na kunufaisha nchi za bara hilo. Anasema, "Kuna tofauti kubwa kati ya hali halisi na kumbukumbu tunayoipata kutoka vitabu kuhusu China. Miundombinu ya kisasa haikuwepo nchini China mwaka 1978. Mfano mzuri zaidi ni mji wa Shenzhen. Zamani Shenzhen ilikuwa kijiji kidogo cha wavuvi, lakini sasa limekuwa jiji kubwa lenye majengo makubwa zaidi kuliko Washington Marekani. Natoa mfano huo ili kukwambia mafanikio ya sera ya mageuzi na kufungua mlango ya China, na nina mifano mengine mingi. China ilivutia uwekezaji na teknolojia kutoka nchi za nje kwa kuanzisha maeneo maalumu ya kiuchumi. Baadaye China ilijifunza kwa makini mpaka imekuwa na rasilimali kubwa."

    Mwaka 1978, China iliingia kwenye zama mpya ya kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, na kuboresha njia ya kusaidia na kushirikiana na nchi za Afrika, ili kuleta manufaa halisi na ufanisi mkubwa zaidi. Hatua mpya za kuzisaidia nchi za Afrika ilikuwa ni kutuma vikundi vya madaktari. Bibi Su Xingman mwenye umri wa miaka 84 alikuwa mkurugenzi wa kitengo cha wanawake cha Hospitali ya Nne ya mkoa wa Hebei, China. Alifanya kazi nchini Zaire ambayo sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo mwaka 1985 na 1986. Hadi sasa anakumbuka vizuri mambo mengi yaliyotokea kwenye hospitali ya Mama Mobutu aliyofanya kazi nchini humo. Anasema,

    "Nilichoka baada ya kumaliza upasuaji, nikawaambia wenzangu waniache nipumzike kwa dakika 20. Wenyeji waliponiona walisema 'China, China' ili kunikaribisha. Baadhi ya wanawake waliwawapa watoto wao waliozaliwa kwenye hospitali yetu jina la 'Su' ambalo ni jina langu la ukoo. Hata rais wao alikutana nami."

    Katika karne mpya, China na nchi nyingi za Afrika zilianzisha uhusiano wa wenzi wa kimkakati. Kutokana na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, China imeanzisha miradi mingi mpya ya ushirikiano ikiwemo "mpango wa pamoja wa urafiki wa China na Afrika", "tamasha la vijana wa China na Afrika", na "mfuko wa uendelezaji wa nguvukazi wa Afrika.

    Bw. Peter Gikonyo ni mwalimu mwenyeji wa lugha ya kichina wa taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Nairobi cha Kenya. Anaona kuelewa utamaduni wa China ni mkondo mpya kwa Kenya, na kujifunza kichina kutasaidia wakenya kupata kazi nzuri. Anasema

    "Naitwa Bi De, na hili ni jina langu la kichina. Nilijifunza lugha ya kichina kwa miaka minne. Zamani nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, halafu nilienda kusoma China, na sasa mimi ni mwalimu wa chuo hicho. Nafundisha lugha ya kichina hapa baada ya kuhitimu masomo yangu mwezi Juni mwaka huu. Kujifunza kichina kumeniletea kazi nyingi, kwa mfano naweza kuwa mkalimani na mwongoza watalii, kwani hivi sasa kuna watalii wengi kutoka China. Nimewaongoza kutembelea mbuga za wanyama za Masai Mara, Amboseli, Samburu na nyinginezo. Mbali na hayo, kuna wachina wengi wanaofanya miradi ya ujenzi au biashara hapa Kenya, pia wanahitaji wakenya wanaojua kichina, na pia nimewasaidia kuwasiliana na wenyeji."

    Kufuatia pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja", China imetekeleza "hatua nane" zilizotolewa na rais Xi Jinping wa China kwenye Mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka jana mjini Beijing, kwa lengo la kuzisaidia nchi za Afrika kuwafundisha watu wenye vipaji vya aina mbalimbali, kuunda mtandao wa kutoa teknolojia, kuhimiza mawasiliano ya sayansi na teknolojia na ushirikiano wa ujasiriamali na uvumbuzi, na kuinua uwezo wa kujiendeleza. Profesa Robert Gituru wa kituo cha utafiti wa pamoja wa China na Afrika anaona kuwa, utafiti wa kituo hicho utasaidia serikali ya Kenya kutunga sera na kuchukua hatua madhubuti katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuzuia uchafuzi wa maji. Anasema,

    "Vifaa hivi vinaendeshwa na kituo cha utafiti wa pamoja wa China na Afrika pamoja na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Kilimo cha Jomo Kenyatta. Lengo la kuanzisha kituo hicho ni kuhimiza ushirikiano kati ya watafiti wa Kenya na nchi nyingine za Afrika na watafiti wa China, kufanya uvumbuzi na kutengeneza bidhaa mpya, ili kuzisaidia nchi za Afrika, China na nchi nyingine duniani kukabiliana na changamoto mbalimbali. Aidha, tuna maabara moja ya utafiti wa maji, ambayo ni moja ya maabara zetu muhimu zaidi. Licha ya Afrika, dunia nzima inakabiliwa na usalama wa maliasili ya maji, hivyo kujenga maabara hiyo kuna maana kubwa kwa juhudi zetu za kuhifadhi raslimali ya maji."

    Katika miaka 70 iliyopita, mabadiliko makubwa yametokea nchini China. Uzoefu wa maendeleo ya China unaweza kuigwa na nchi nyingi za Afrika. Balozi wa Kenya nchini China Bibi Sarah Sarem alipohojiwa na wanahabari wa radio yetu alisema, Chama cha Kikomunisti cha China kimewaongoza wananchi wa China kupata mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu na kuondoa umaskini, na kutoa mfano mzuri kwa nchi za Afrika ikiwemo Kenya. Anasema, 

    "Miaka 70 iliyopita, hakukuwa na mtandao wa kisasa wa reli kama ilivyo sasa nchini China, wala mtandao wa safari za ndege. Kenya inaiheshimu China kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuboresha miundombinu na maisha ya watu, na kuendeleza viwanda, na kutaka kunufaika na uhusiano mzuri kati yake na China. Uzoefu mwingine wa China unaostahili kuigwa na Kenya ni kwamba, japo serikali za mitaa za China zina uhuru wa kujiamulia mambo yao na mikakati tofauti ya kuendeleza uchumi, lakini sera zao zinalingana vizuri na sera ya serikali kuu, na hali hii imeleta mshikamano mzuri nchini China."

    Nchi za Afrika ni wenzi wa kiasili ya pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja", na hadi sasa zaidi ya nchi 40 barani Afrika zimejiunga na ujenzi wa pamoja wa pendekezo hilo. Miradi ya ujenzi wa reli, barabara, madaraja, uwanja wa ndege, bandari na maeneo ya viwanda iliyotekelezwa barani Afrika kufuatia pendekezo hilo imeleta ufanisi mkubwa wa kijamii. Mkuu wa kiongozi wa ujumbe wa China katika Umoja wa Afrika Bw. Liu Yuxi amesema, mkutano wa pili wa kilele wa ushirikiano wa kimataifa wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja ulifanyika Aprili mwaka huu mjini Beijing kwa mafanikio makubwa, na kufungua ukurasa mpya wa ujenzi wa pamoja wa sifa ya juu wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja". Mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu mjini Addis Ababa, Ethiopia, ujumbe wa China katika Umoja wa Afrika pia uliandaa kongamano la ushirikiano wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja" kati ya China na Afrika, na kufuatiliwa sana na pande mbalimbali za Afrika. Anasema,

    "Ushirikiano wa 'Ukanda Mmoja, Njia Moja' ni matarajio ya pamoja ya watu wa China na Afrika, na umeleta manufaa halisi na kutia uhai na injini mpya kwenye uhusiano wa wenzi na ushirikiano wa kimkakati kwa pande zote kati ya China na Afrika. Katika siku zijazo, China itafuata kanuni ya kushauriana, kujenga kwa pamoja na kunufaika kwa pamoja, na mawazo ya kufungua mlango, kutoleta uchafuzi kwa mazingira na bila kuwepo kwa ufisadi, kuzingatia malengo endelevu yenye vigezo vya juu ya kuboresha maisha ya watu, na kukaribisha nchi nyingi zaidi za Afrika kushiriki kwenye ujenzi wa 'Ukanda Mmoja, Njia Moja', ili kunufaika kwa pamoja na fursa ya kihistoria na kuhimiza ushirikiano halisi. China pia inapenda kuimarisha mawasiliano ya kisera na nchi za Afrika, na kutunga mipango ya pamoja ya ushirikiano, na kuunganisha vizuri pendekezo la 'Ukanda Mmoja, Njia Moja' na ajenda ya mwaka 2063 ya maendeleo ya Afrika. Aidha, China itafuata mwelekeo wa ujenzi wa eneo la biashara huria na mafungamano ya kikanda barani Afrika, kurahisisha biashara na uwekezaji kati ya China na Afrika, na kujenga mifumo anuwai na endelevu ya mitaji. Zaidi ya hayo, China itajitahidi kutafuta ushirikiano mpya mzuri na Afrika katika sekta za miundombinu, nishati, kilimo, afya, na TEHEMA, na kuimarisha zaidi mawasiliano na ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika utamaduni, elimu, washauri mabingwa, na utalii, ili kujenga daraja la kirafiki la kuhimiza staarabu tofauti kufunzana, na watu kuelewana, na kuunga mkono ujenzi wa pamoja wa 'Ukanda Mmoja, Njia Moja'."

    Katika siku zijazo, China itaendelea kushikilia nia yake ya awali ya kuwa na urafiki dhati na kutendeana kwa usawa, kushirikiana na nchi za Afrika kutetea utaratibu wa pande nyingi na mafungamano ya uchumi duniani, kupunguza pengo la ustaarabu kupitia mawasiliano, kuacha migogoro ya ustaarabu kupitia kufundishana, na kuondoa mawazo ya kujigamba kistaarabu kwa kusikilizana na kuishi kwa pamoja, ili kutoa mchango zaidi kwa ajili ya ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakbali wa pamoja.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako