Wakenya Brigid Kosgei na Lawrence Cherono walitawala mbio za kifahari Jumapili za Chicago Marathon nchini Amerika, huku Kosgei akivunja rekodi ya dunia ya wanawake ya Paula Radcliffe ya saa 2:15:25 iliyokuwa imedumu tangu mwaka 2003. Kosgei alinyakua taji lake la pili mfululizo la Chicago kwa saa 2:14:04 katika mbio hizi zilizovutia watimkaji 45,000. Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 25 aliongoza mbio hizi kutoka mwanzo hadi utepeni. Alivunja pia rekodi ya dunia ya wanawake pekee ya saa 2:17:01 ambayo Mkenya mwenzake Mary Keitany aliweka jijini London mwaka 2017. Alifuta rekodi ya Chicago Marathon ya wanawake ya saa 2:17:18 ambayo Radcliffe aliweka mwaka 2002.