• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Nchi za Afrika zajitahidi kutatua msukosuko wa chakula

  (GMT+08:00) 2019-10-16 18:20:51

  Leo ni Siku ya Chakula Duniani, na kauli mbiu ya mwaka huu ni "vitendo vyetu ni mustakbali wetu, vyakula vya afya kwa ajili ya dunia isiyo na Njaa". Hivi sasa kwa ujumla, hali ya usalama wa chakula duniani inaboreshwa, lakini bado inakabiliwa na changamoto, ambapo tatizo la njaa linalozikabili nchi za Afrika limejitokeza zaidi. Hata hivyo nchi za Afrika hazijashindwa na msukosuko wa chakula, bali zinaongeza juhudi ili kutimiza usalama wa chakula na maendeleo endelevu mapema iwezekanavyo.

  Ripoti iliyotolewa mwezi Julai na Umoja wa Mataifa inasema, uwiano wa watu wenye njaa duniani ulipungua kwa mfululizo katika miongo kadhaa iliyopita, na kimsingi umedumisha chini ya asilimia 11 baada ya mwaka 2015, lakini idadi halisi ya watu wenye njaa inaongezeka na kufikia zaidi ya milioni 820 mwaka jana.

  Ofisa wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia masuala ya kilimo na vijiji Janet Edeme alisema kwenye mkutano kuhusu chakula uliofanyika mwezi Septemba kuwa, Afrika ni bara linalokosa zaidi usalama wa chakula duniani, na kila mmoja kati ya watu wanne ana utapiamlo. Idadi ya watu wa Afrika inatarajiwa kufikia bilioni 2.5 ifikapo mwaka 2050, ambapo usalama wa chakula utakabiliwa na changamoto kubwa zaidi.

  Zimbabwe na Sudan Kusini ni nchi zinazokabiliwa na msukosuko mbaya zaidi wa chakula barani Afrika. Mwezi Machi, Katibu mkuu wa kudumu wa Wizara ya Huduma za Umma, Kazi na Ustawi wa Jamii nchini Zimbabwe Judith Kateera alisema, kutokana na ukame unaosababisha upungufu wa mavuno na sababu nyingine, inatarajiwa kuwa mwaka huu watu zaidi ya milioni 7 nchini mwake watakabiliwa na upungufu wa chakula, idadi hii inachukua asilimia zaidi ya 40 ya watu wote wa nchi hiyo.

  Mjumbe wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP nchini Sudan Kusini Matthew Hollingworth amesema, watu milioni 6.35 wa Sudan Kusini wanakabiliwa na msukosuko wa usalama wa chakula, idadi ambayo imechukua nusu ya watu wote wa nchi hiyo.

  Wachambuzi wamesema sababu za msukosuko wa chakula katika nchi za Afrika ni za kiasili, kijamii na kiuchumi.

  Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Ubinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema, kutokana na hali mbaya ya hewa, katika miaka ya hivi karibuni, Afrika inazidi kukabiliwa na changamoto ya chakula. Katika msimu wa mvua wa kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2019, kiwango cha mvua zilizonyesha katika sehemu nyingi za kusini mwa Afrika kilikuwa cha chini zaidi katika miaka 40 iliyopita.

  Mbali na athari ya mabadiliko ya hali ya hewa, umaskini, ugonjwa wa UKIMWI, ukosefu wa ajira na hali mbaya ya uchumi pia ni sababu za kuongezeka kwa makali ya msukosuko wa chakula. Wakati huohuo, hasara na ubadhirifu katika uzalishaji, usindikaji, usambazaji, uhifadhi na ulaji wa chakula pia havipaswi kupuuzwa. Kwa mujibu wa Bibi Janet Edeme, katika eneo la Afrika kusini mwa Sahara, hasara ya chakula inatarajiwa kufikia zaidi ya tani milioni 100 kila mwaka, kiasi ambacho kinalingana na mahitaji ya chakula kwa watu milioni 48 kila mwaka.

  Umoja wa Afrika na nchi za Afrika zinajitahidi kuchukua hatua kukabiliana na msukosuko mbaya wa chakula. Hivi sasa "Mpango wa Maendeleo wa Jumla wa Kilimo wa Afrika" uliopitishwa na Umoja wa Afrika mwaka 2003 unaendelea kutekelezwa kwa kasi. Matokeo ya utekelezaji wa miaka zaidi ya kumi yameonyesha kuwa mpango huo umehimiza maendeleo ya kilimo cha Afrika, na ongezeko la kiwango cha wastani cha mwaka cha kilimo limekuwa dhahiri kuliko miongo kadhaa kabla ya hapo.

  Aidha, Ajenda ya Mwaka 2063 iliyotolewa na Umoja wa Afrika mwaka 2015, na mpango wa kwanza wa miaka kumi umedhihirisha mpango mkubwa wa kuongeza kasi ya maendeleo ya viwanda na kutimiza lengo la kujitosheleza kwa chakula.

  Mbali na juhudi za nchi za Afrika zenyewe, msaada kutoka jamii ya kimataifa pia hauwezi kukosekana. Tokea mwaka huu uanze, ili kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na msukosuko wa chakula, serikali ya China imetoa msaada wa chakula wa dharura kwa Somalia, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi nyingine. Vilevile hadi mwaka 2016, China ilikuwa imezisaidia nchi zaidi ya 50 za Afrika kutekeleza miradi zaidi ya 500 ya kilimo, ambayo inahusu ukulima, uhifadhi wa chakula, mashine za kilimo, umwagiliaji na usindikaji wa mazao ya kilimo. China siku zote inatilia mkazo kufanya ushirikiano na Afrika katika sekta ya kilimo, kutekeleza miradi ya msaada ya kilimo, na kuzisaidia nchi za Afrika kutimiza usalama wa chakula na maendeleo endelevu.

  Janet Edeme anasema, China imepata mafanikio makubwa katika kupunguza umaskini kupitia sekta ya kilimo, na ina uzoefu wa kisasa katika usimamizi wa chakula na usindikaji wa mazao ya kilimo, ambao unastahili kuigwa na nchi za Afrika.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako