Kufuatia kuonesha mchezo safi katika michuano ya kabla ya msimu wikiendi iliyopita, baada ya kuwagaragaza mabingwa wa ligi Rwanda Energy Group (REG), UTB imeapa kulianzisha dude katika msako wake wa kulitia mkononi kwa mara ya kwanza taji la ligi ya mpira wa wavu nchini Rwanda. Ligi ya mpira wa wavu taifa kwa msimu wa 2019/2020 itaanza kutimua vumbi Jumamosi. Fidele Nyirimana kocha aliyejiunga na UTB mwaka jana akitokea Gisagara amesema wanaanza kampeni zao za kulisaka taji dhidi ya mabingwa mara mbili Gisagara, IPRC-West na APR wikiendi hii. Amesisitiza kuwa baada ya miaka michache kwenye ligi, anaona sasa wamepevuka vya kutosha kuweza kunyanyua kombe. Amesema mashindano ya kabla ya msimu yamemsaidia kuwatathmini wachezaji wake hivyo ana imani nao. Baada ya kumaliza wa tatu katika msimu uliopita, UTB imekuwa bize kwenye soko la uhamisho ambapo wamesaini wachezaji watatu mshambuliaji wa kulia Nelson Murangwa, mshambuliaji wa kushoto Olivier Ntagengwa na mzuiaji wa kati Fred Musoni.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |