Kundi la mwisho la wachezaji wa Harambee Stars wanaosakata kabumbu ya kulipwa ughaibuni, liliwasili juzi nchini Misri ili kuungana na wenzao, kwa mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021. Fainali hizo zitaandaliwa nchini Cameroon mwaka 2021. Stars watakabiliana na Misri leo Alhamisi katika mechi ya ufunguzi wa Kundi G chini ya kocha Francis Kimanzi, Stars watashuka ugani Borg El Arab jijini Alexandria kuvaana na Misri, ambao walikuwa wenyeji wa makala iliyopita ya AFCON, ambayo ubingwa wake ulitwaliwa na Desert Foxes ya Algeria. Baada ya kukamilisha kibarua hicho kigumu dhidi ya Misri, ambao ni bingwa mara saba wa AFCON, Harambee watakuwa wenyeji wa Togo katika mchuano wa pili uwanjani MISC Kasarani, Nairobi. Mchuano huo utachezwa Novemba 18. Wakati huohuo Harambee Stars wamepewa hadi leo usiku kulipa gharama za hoteli wanayokaa jijini Cairo ama watimuliwe. Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirkisho la Soka nchini (FKF) Barry Otieno amesema, kumekuwapo na ahadi kutoka Wizara ya Michezo tangu Ijumaa, Novemba 8, lakini ahadi hizo zimekuwa ni maneno matupu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |