BASKETBALL: Bandari, Storms watia fora vikapuni
(GMT+08:00) 2019-11-19 17:15:19
Timu za mpira wa vikapu za Bandari na Storms za Kenya zimeingia nusu-fainali ya Ligi Kuu ya wanawake baada ya kung'aa katika robo-fainali jijini Nairobi, wikendi. Bandari waliwabanjua wenyeji wao Eagle Wings 2-0 katika mfululizo wa mechi tatu za robo-fainali. Ilifunga Wings 78-43 katika mechi ya kwanza Jumamosi. Bandari, ambayo ilipoteza ubingwa kwa kulazwa 3-1 dhidi ya Equity Bank katika fainali ya mwaka jana, haikulegeza kamba katika mechi ya pili ambapo ililaza Wings 79-31 Jumapili. Storms,iliyokamilisha msimu wa kawaida katika nafasi ya sita, ilianza robo-fainali kwa kushindwa 42-39 na Strathmore. Hata hivyo, Storms ya kocha Abel Nson iliamka katika mechi ya pili na kushinda 70-54. Storms ilimaliza katika nafasi ya tatu mwaka jana.