• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wajasiriamali EAC wafaidika na mafunzo ya biashara China

    (GMT+08:00) 2019-11-25 08:18:56

    MAONESHO ya wajasiriamali wa sekta isiyo rasmi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imewezesha wafanyabiashra hao wadogo kutembelea China kujifunza namna bora ya kuboresha shughuli zao za kiuchumi.

    Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema hayo Jumapili, Novemba 24, 2019, wakati akifunga Maonesho ya Wajasiriamali wa Tanzania kusherehekea miaka 20 ya uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Fumba, Zanzibar.

    Alibainisha kuwa maonesho hayo yanalenga kuwafunza wajasiriamali mbinu mbalimbali za namna ya kuboresha biashara na kutoa fursa ya mafunzo kwa nchi zilizoendelea na kuwa na mafanikio makubwa katika biashara.

    "Wajasiriamali hawa wameweza kufanya ziara katika nchi ya China ambako walijifunza na kununua mashine za kisasa kwa ajili ya kuboresha uzalishaji wa bidhaa zao ili ziweze kushindana katika soko la ndani na la nje," alisema Majaliwa.

    Aliongeza kuwa maonesho hayo yanasaidia kuwawapatia wajasiriamali uthubutu wa ushiriki wao binafsi katika maonesho mengine kwenye nchi za Afrika Kusini, Malawi, Zambia, Sudan Kusini, Msumbiji na Marekani.

    Waziri mkuu Majaliwa alisema wanapohitimisha maonesho hayo sambamba na kusherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatakiwa wajitathmini kuona kama wametimiza malengo ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.

    "Vilevile, tuendeleze ujirani mwema, kupanua na kuimarisha ushirikiano wa watu wa Afrika Mashariki ili kuharakisha ukuaji wa kiuchumi sanjari na kuboresha maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki kiuchumi, kisiasa na kijamii."

    China ni mbia mkubwa wa Maendeleo kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa sekretareti ya EAC pamoja na kwa nchi wanachama.

    Hivi karibuni Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ilitoa msaada wa magari 12 yenye thamani ya Dola za Kimarekani 400,000 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za sekretarieti ya EAC.

    Pamoja na msaada wa magari, nchi hiyo ya pili kwa utajiri duniani pia ilitoa jumla ya Dola za Kimarekani 200,000 kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi sektetarieti hiyo yenye makao yake makuu jijini Arusha, Tanzania.

    Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzungumzia kuhusu vikwazo visivyo vya kiforodha vinavyozorotesha wajasiriamali kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

    Alisema vikwazo hivyo na changamoto mbalimbali za kibiashara vimeendelea kutatuliwa kupitia majadiliano baina ya Tanzania na nyingine ndani ya Jumuiya hiyo kwa lengo la kuvipunguza na kuviondoa kabisa.

    Waziri Mkuu amesema kupitia majadiliano hayo, Serikali ya Tanzania imefanikiwa kuratibu zoezi la uondoaji wa vikwazo vya biashara visivyo vya kiforodha 15 kati ya 24 vilivyoripotiwamwaka 2019 navikwazo tisa vilivyobakiahatua ya kuvipatia ufumbuzi inaendelea.

    Hata hivyo,Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutekeleza mkakati wa kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha wajasiriamali wanachangamkia fursa za kibiashara zitokanazo na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

    Waziri Mkuu amesema mkakati huo unahusisha zoezi la kufanya utafiti wa uelewa wa Watanzania kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki na matokeo ya utafiti huo yatatumika katika kutoa elimu kwa umma kulingana na mahitaji.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako