Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' wamepangwa Kundi C kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge inayotaraiwa kuanza Desemba 7 hadi 19 mjini Kampala nchini Uganda. Kilimanjaro Stars, mabingwa wa 1975, 1994 na 2010 wamepangwa pamoja na ndugu zao, Zanzibar 'Heroes', Djibouti na mabingwa watetezi, Kenya 'Harambee Stars'. Kundi A linaundwa na wenyeji, Uganda, Burundi, Ethiopia na Eritrea, wakati Kundi B linaundwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Sudan, Sudan Kusini na Somalia. Uganda ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara saba, Ethiopia mara nne na Tanzania mara tatu. Mara ya mwisho Tanzania Bara ilitwaa Kombe hilo mwaka 2010 jijini Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha Mdenmark, Jan Borge Poulsen.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |