• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Umoja wa Afrika watoa mwito wa kukabiliana na mzigo unaosababishwa na ugonjwa wa UKIMWI kwa makundi dhaifu

  (GMT+08:00) 2019-12-02 08:49:36

  Mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika Bw. Moussa Mahamat ametoa wito wa kuwepo kwa juhudi za makusudi kupunguza mzigo wa ugonjwa wa UKIMWI kwa watu wazima walioko kwenye makundi yaliyo hatarini, hasa wakimbizi, watu wanaorudi makwao na wakimbizi wa ndani.

  Akiongea jana wakati wa maadhimisho ya siku ya kupambana na UKIMWI duniani, Bw. Mahamat amesema makundi hayo yako hatarini zaidi, kama ilivyo kwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 na miaka 19, ambao wako kwenye hatari kubwa ya maambukizi mapya. Bw. Mahamat pia amesema kuna haja ya haraka na kuweka mkazo kwenye kukabiliana na uhusiano kati ya maambukizi ya virusi vya UKIWMI na mabavu ya kijinsia, hasa kwenye mazingira ya kibinadamu na kwenye migogoro.

  Siku hiyo imeadhimishwa wakati kukiwa na habari za kuridhisha kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI, licha ya changamoto zinazoendelea kuwepo katika nchi mbalimbali. Nchini Afrika Kusini, Naibu Rais wa nchi hiyo Bw. David Mabuza amesema Afrika Kusini sasa inauchukulia ugonjwa wa UKIMWI kuwa ni hatari ya afya kwa umma, na inapanga kutokomeza ugonjwa huo kabla ya mwaka 2030. Hata hivyo amesema safari ya kuhakikisha hakuna maambukizi mapya, hakuna unyanyapaa na hakuna vifo imekuwa ndefu na ngumu.

  Nchini Tanzania habari zinasema Waziri wa nchi Ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia sera, bunge, nguvu kazi, ajira, vijana na walemavu Bibi Jenister Mhagama, amesema vijana hasa wasichana ndio wanaongoza kwenye maambukizi mapya. Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Mwanza, Bibi Mhagama amesema utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuwa utafiti uliofanywa mwaka 2016-2017 unaonesha kuwa kulikuwa na maambukizi mapya elfu 72 ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24, kati ya hayo asilimia 80 walikuwa ni wasichana na asilimia 20 walikuwa ni wavulana. Kwa ujumla watu milioni 1.4 nchini Tanzania wanaishi na virusi vya UKIMWI.

  Ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupambana na ugonjwa huo, China imepata maendeleo makubwa kwenye kazi ya kinga na tiba ya ugonjwa wa UKIMWI na kufanikiwa kudhibiti maambukizi katika kiwango cha chini. Kamati ya taifa ya afya ya China imesema maambukizi kupitia kuongezewa damu kimsingi yamekomeshwa, na maambukizi kupitia kujidunga dawa za kulevya na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamezuiwa kwa ufanisi. Hadi kufikia mwezi Oktoba idadi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI nchini China ilikuwa laki 9.58, na katika miezi 10 ya mwanzo wa mwaka huu kulikuwa na maambukizi mapya laki 1.3. Kwa sasa kamati ya afya imesema imeweka mpango wa kupambana na maambukizi kupitia njia ya kujamiana, ambayo ndio njia kuu kwa sasa, na kutokomeza kabisa maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako