Mashabiki wengi wa ngumi wanajiuliza maswali namna Hassan Mwakinyo alivyocheza na kushinda dhidi ya Arnel Tinampay usiku wa Ijumaa iliyopita kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam. Mwakinyo ambaye baada ya pambano hilo alikiri kushinda kwa tabu kwa matokeo ya pointi, ameanika namna glovu zilivyomponza ulingoni. Baada ya kupanda ulingoni, mashabiki walilazimika kusubiri kwa zaidi ya dakika 10 huku Mwakinyo akijaribishwa glovu tofauti na kuvuliwa akiwa ulingoni. Mwakinyo alisema ilikuwa ni changamoto ambayo wengi hawaijui, lakini glovu alizopigania zilikuwa zinambana na kushindwa hata kukunja ngumi ipasavyo. Anasema licha ya kumbana, lakini pia zilitoka kutumika kwenye mapambano ya utangulizi hivyo zilikuwa na jasho, lakini alilazimika kucheza hivyo hivyo ili kutoonekana tofauti kwa mashabiki waliofurika uwanjani kumshuhudia. Naye bingwa wa zamani wa super-bantamweight wa WBC Fatuma Zarika atapambana na Mbulgarian Ilvanka Ivanova kwenye pambano lisilo na taji Disemba 13 katika Charter Hall, Nairobi. Hii itakuwa ni nafasi nzuri kwa Zarika anayetaka kujiandaa na mechi ya kurejeana dhidi ya bingwa wa WBC super-bantamweight Mmexico Yamileth Mercado Machi mwakani. Katika pambano la mwezi uliopita huko Chihuahua, Mercado alimtoa kijasho Zarika katia raundi zote tatu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |