SOKA: Wachezaji saba kutoka timu ya taifa ya soka ya Eritrea wazamia nchini Uganda
(GMT+08:00) 2019-12-27 10:13:25
Wachezaji saba kutoka timu ya taifa ya soka ya Eritrea wameingia mitini baada ya kucheza kwenye mashindano nchini Uganda. Hii ni mara ya pili ndani ya miezi miwili wachezaji wa soka kutoka nchi hiyo kupotea wakati wakitembelea Uganda. Hakuna taarifa zozote juu ya walipokwenda. Lakini katika muongo mmoja uliopita wanariadha kadhaa wamekuwa wakikataa kurudi nyumbani au kukimbia wakati wanaposhindana nchi za nje, mara nyingi wakidai hifadhi. Kwa mujibu wa msemaji wa shirikisho la soka la Afrika Mashariki CECAFA Rogers Mulindwa, wachezaji hao saba walikuwa na ulinzi mkali hotelini walikofikia siku ya Jumatatu. Hadi sasa hakuna tamko lolote lililotolewa na serikali ya Eritrea kuhusiana na tukio hilo. Wachezaji waliosalia walirudi nyumbani baada ya kushindwa na Uganda 3-0 kwenye michuano ya CECAFA Senior Challenge.