• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Matukio mengi makubwa yaliyojiri katika ulimwengu wa michezo

    (GMT+08:00) 2019-12-31 08:42:16

    Zikiwa zimesalia saa chache tu kuugaka mwaka 2019 kuna matukio mengi makubwa yaliyojiri katika ulimwengu wa michezo. Na hapa nimejaribu kukudondolea mawili matatu. Nikianza na kombe la mataifa ya Afrika lililochezwa nchini Misri kwa mara ya kwanza fainali za kombe hilo zilishirikisha mataifa 24 .

    Kwa mara ya kwanza Afrika mashariki ikawakilishwa na timu 4 ambazo ni Burundi iliyoshiriki kwa mara ya kwanza, Tanzania, Kenya na Uganda, lakini kubwa zaidi ilikuwa Tanzania kushiriki katika kundi moja na Kenya ambazo ni watani wa jadi hata kuanzia ngazi ya CECAFA.

    Mbali na michuano mingine ya kombe la AFCON, Mchezo kati Kenya na Tanzania nao ulizungumzwa sana kama dabi ya Afrika mashariki.

    Hatimaye, Kenya ikaibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 3-2 na kuwafurahisha mashabiki wa Kenya walioshuhudia pambano hilo:

    Kwa upande wake nahodha wa Taifa Stars ya Tanzania Mbwana Samatta alihuzunishwa na jinsi walivyopoteza pambano hilo ilihali walikuwa mbele kwa bao 2.

    Timu ya Tanzania imeshiriki michuano hiyo baada ya kipindi cha miaka 39 kupita bila ya taifa hilo kushiriki fainali za kombe la Afrika la mataifa:

    Hatimaye timu nyingine zilizokuwa katika kundi hilo Senegal na Algeria zilikutana katika fainali na Algeria ikaibuka kidedea kwa kushinda bao 1 bila na kutawazwa mabingwa wa Afrika.

    Mbali na soka, mwaka huu unaomalizika pia ulitawaliwa na riadha kubwa zaidi ni mwanariadha wa Kenya Eliud Kipchoge kuweka muda bora zaidi chini ya saa mbili katika mbio za Marathon huko Ineos .

    Matukio mengine ya riadha, Urusi imefungiwa kwa miaka minne kushiriki michezo yoyote mikubwa ya kimataifa na wakala wa kupambana na dawa za kusisimua misuli (Wada).

    Ina maanisha kuwa bendera ya Urusi haitapepea wala wimbo wao wa taifa wa nchi yao hautapigwa kwenye michuano kama ya Olimpiki ya mwaka 2020 na michuano ya kandanda ya kombe la dunia ya mwaka 2022 nchini Qatar.

    Na mwisho kabisa, Kenya yamaliza ya pili baada ya Marekani katika mashindano ya riadha ya duniani.

    Kama ilivyokuwa mwaka 2017 wakati wa mashindano kama haya, wakati yalipofanyika jijini London nchini Uingereza, Marekani imemaliza ya kwanza, huku Kenya ikiwa ya pili.

    Marekani iliongoza kwa kupata medali 29, zikiwemo 14 za dhahabu, 11 za fedha na 4 za shaba.

    Kenya ilimaliza mashindano hayo kwa kupata medali 11, zikiwemo tano za dhahabu mbili za fedha na nne za shaba.

    Miongoni mwa wanariadha wa Kenya waliopata medali ya dhahabu ni pamoja na Hellen Obiri mbio za Mita 5,000 kwa upande wa wanawake na Conseslus Kipruto Mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

    Na sasa nawapisha wenzangu Pili Mwinyi na Fadhili Mpunji wakiangalia mastaa wa Kiafrika waliofanya vizuri katika mwaka 2019.

    Zikiwa zimebaki saa kadhaa tu kuumaliza mwaka 2019 ambao ulikuwa na matukio mengi ya kimichezo, tuangalie kikosi cha mastaa wa Kiafrika waliofanya vizuri ndani ya siku 365 za mwaka huu katika ligi mbalimbali za mataifa makubwa barani Ulaya. Katika orodha ya mastaa mbalimbali wa Afrika ambao wanaonekana kuwa katika kiwango bora zaidi kwa sasa ni Mohamed Salah na Sadio Mane wa Liverpool ambao wanatoka katika ukanda wa Afrika Mgharibi katika mataifa ya Senegal na Misri. Kutoka ukanda wa Afrika Mashariki anayeonekana kuwa katika kiwango bora zaidi ni nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta ambaye amefanya vizuri akiwa na KRC Genk.

    Hii hapa orodha kamili ya mastaa wa Afrika ambao wamekamua ile mbaya ndani ya mwaka huu. Kikosi hiki kinaundwa kwa kuzingatia mfumo wa 4-1-3-2 huku kikiwa na kiungo mkabaji mmoja kiasili ambaye ni Ndidi.

    ANDRE ONANA Licha ya kuwa Ajax, imeondolewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuhamia upande wa Europa Ligi, Onana ambaye ni raia wa Cameroon, amekuwa katika kiwango bora ndani ya michezo 18 ya Ligi Kuu Uholanzi 'Eredivisie' amefungwa mabao 16 na hajaruhusu bao katika michezo sita. Ubora wa kiwango chake umekuwa ukitajwa kuchangiwa na akademi ya FC Barcelona ambayo alipitia kabla kutua Ajax, Juni 14, 2015.

    SERGE AURIER - Panga pangua katika ubavu mmoja wa kikosi cha Tottenham yani beki ya pembeni amekuwa akicheza, Aurier. Msimu huu katika michezo 15 ya Ligi Kuu England ambayo amecheza hajafunga bao hata moja lakini ame-assisti mabao matatu, japo juzi amejifunga moja katika sare ya 2-2 dhidi ya Norwich. Kwa sasa ameonakana kurejea katika makali yake kwani msimu uliopita alikuwa akikabiliwa na changamoto ya namba katika kikosi cha kwanza kiasi cha kuanza kuhusishwa kuwa na mipango ya kutimka katika jijini la London.

    RAMY BENSEBAINI

    Ni beki wa kushoto wa Borussia Mönchengladbach, amekuwa akifanya vizuri. Bensebaini ambaye ni Mualgeria amecheza michezo minane msimu huu wa Ligi Kuu Ujerumani na kufunga mabao matatu na kuassisti moja. Upande wa Europa Ligi alitumika katika michezo yote sita ya hatua ya makundi. Licha ya uwepo wa Faouzi Ghoulam ambaye naye ni Mualgeria anayeichezea Napoli, Bensebaini anabaki kama beki bora zaidi wa kushoto kwa Afrika kutokana na kiwango alichokionyesha. Ghoulam hajawa na nafasi ya kucheza mara kwa mara akiwa na Napoli. Beki huyo wa kushoto, amecheza mechi tano tu za Ligi Kuu Italia ambayo ni maarufu kama Serie A, hajafunga wala kuassisti katika mchezo wowote hivyo takwimu zinamuangusha mbele ya Mualgeria mwenzake.

    JOEL MATIP

    Amekuwa mmoja wa walinzi makini licha ya kuwa alijiunga na majogoo wa jiji Liverpool bure. Matip kwa sasa ni majeruhi lakini amekuwa akicheza na Virgil van Dijk kama mabeki pacha wa kati yani nne na tano katika kikosi hicho cha Jurgen Klopp. Wacameroon kwa sasa hawataki hata kumsikia, wanamwona msaliti kutokana na beki huyo wa kati kukataa wito wa taifa hilo msimu miwili iliyopita alipoitwa kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika. Bila ya Matip, Cameroon walichukua ubingwa wa Afcon tangu hapo hakuitwa tena.

    KALIDOU KOULIBALY

    Koulibaly ambaye ni Msenegal ni miongoni mwa mabeki bora duniani, amecheza michezo 14 ya Ligi Kuu Italia 'Serie A' na michezo yote sita ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya makundi akiwa na klabu yake ya Napoli.

    WILFRED NDIDI

    Kiwango ambacho amekionyesha kiungo huyo wa Nigeria ndani ya mwaka huu katika klabu yake ya Leicester City, kimeanza kuzivutia klabu mbalimbali kubwa nchini England, ikiwemo Arsenal. Amekuwa mhimili wa eneo la kiungo mkabaji katika kikosi cha Brendan Rodgers.

    HAKIM ZIYECH

    Mmoja wa mawinga hatari kwa sasa wa Kiafrika ambaye anafanya vizuri nchini Uholanzi akiwa na Ajax, Ziyech ambaye ni Mmorocco ameifungia klabu yake mabao sita na kutoa assisti 13 katika michezo 17 ya Ligi Kuu nchini humo, iitwayo Eredivisie.

    SADIO MANE

    Licha ya kucheza kama mshambuliaji wa pembeni Mane amekuwa hatari kiasi cha kushindana na washambuliaji wa kati katika vita ya kuwania kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu England. /  Kabla ya mchezo wa jana ambapo alikuwa akiiongoza Liverpool dhidi ya wababe wa Manchester City, Wolves, Mane ameifungia klabu yake mabao tisa na assisti nane katika michezo 17 ya Ligi hiyo.

    MO SALAH

    Anaweza kutokea pembeni kama ilivyo kwa Mane na hata kucheza nyuma ya washambuliaji, ni mzuri kwenye kumalizia na kuassisti naye kabla ya mchezo wa jana, ameifungia Liverpool mabao tisa huku akiwa na assisti nne katika michezo 14 aliyoichezea klabu yake. MBWANA SAMATTA

    Samatta ambaye ametimiza miaka 27 siku chache zilizopita amekuwa katika kiwango bora msimu huu, ameifungia klabu yake ya KRC Genk mabao saba katika michezo 20 ya Ligi Kuu Ubelgiji maarufu kama Jupiler Pro. Upande wa Ligi ya Mabingwa Ulaya licha ya klabu yake kutupwa nje aliifungia mabao matatu, mawili dhidi ya Salzburg huku moja likiwa dhidi ya majogoo wa jiji Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield.

    PIERRE AUBAMEYANG

    Mshambuliaji huyo wa Gabon kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Chelsea, ameifungia Arsenal mabao 12 katika michezo 19 ya Ligi Kuu England huku akiwa na assisti moja. Uzuri wa Aubameyang amekuwa akitoa wigo mpana wa kutumika katika safu ya ushambuliaji ya Arsenal, anaweza kusimama mwenyewe mbele, anaweza kucheza na msaidizi na pia ana uwezo wa kutokea pembeni.

    Tottenham Hotspur ilishtua wadau wa soka ulimwenguni baada ya kumtimua kocha wao Mauricio Pochettino,lakini hiyo haikuwa klabu poekee iliyochukua htua hiyoi mwaka huu katika msimu wa 2019/20. Hapa kuna orodha ya majina makubwa 10 ya mameneja walitimuliwa katika msimu huu. Nayo Bayern Munich ilitoa maamuzi magumu ya kumfukuza Niko Kovac. Mwaka huu pia haukuwa mwema kwa kocha Marco Giampaolo wa AC Milan. Kibarua kingine kilichoota mbawa ni cha kocha Marcelinho wa Valencia, Javi Gracia wa Watford, Sylvinho – Olympique Lyonnais, Igor Tudor – Udinese, Fran Escriba – Celta Vigo, Eusebio Di Francesco – Sampdoria, Jaap Stam – Feyenoord. Manuel Pellegrini wa West Ham United. Unai Emery wa Arsenal.

    Kwa upande wa Afrika

    Clarence Seedorf – Cameroon, Kocha Amunike - Tanzania, Sebastien Desabre wa Uganda ingawa huyu ni kwa ridhaa yake. Javier Aguirre - Misri

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako