• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Iran yashambulia vituo vya kijeshi vya Marekani kwa kulipiza kisasi

    (GMT+08:00) 2020-01-08 18:36:59

    Vikosi vya Ulinzi vya Mapinduzi ya Kiislamu vya Iran IRGC leo alfajiri vimerusha makombora kulenga vituo visivyopungua viwili vya kijeshi vya Iraq vyenye askari wa Marekani.

    Taarifa iliyotolewa na IRGC inasema, mashambulizi hayo ya makombora yaliyofanywa na Iran ni kwa ajili ya kulipiza kisasi dhidi ya Marekani kwa kumuua mkuu wa kikosi cha Quds cha jeshi la Iran Meja Jenerali Qassem Soleimani. Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameitaka Marekani iondoe majeshi yake kutoka kwenye kanda hiyo, akisema mashambulizi ya makombora ni pigo kubwa usoni mwa Marekani, lakini bado hayatoshi.

    Wizara ya ulinzi ya Marekani imethibitisha mashambulizi hayo na kusisitiza kuwa nchi hiyo itafanya linalowezeka kuwalinda Wamarekani, wenzi na washiriki wake katika kanda hiyo. Rais Donald Trump wa Marekani kwenye account yake ya Twitter amesema, hadi sasa nchi yake ina nguvu kubwa zaidi ya kijeshi duniani. Siku moja kabla ya hapo, rais huyo aliionya Iran kuwa kama ikifanya lolote lisilopaswa kufanywa, itakabiliwa na matokeo makubwa mno. Moja ya vituo vilivyoshambuliwa vya Marekani ni kituo cha al-Asad cha jeshi la anga. Kituo hicho kilichoko kilomita 190 kaskazini mashariki mwa Baghdad kilianza kutumiwa na Marekani mwaka 2003 baada ya vita vya Iraq. Kituo hicho kina askari wengi zaidi wa Marekani ikilinganishwa na vituo vingine. Wachambuzi wanaona kuwa, sababu ya Iran kuchagua kituo hicho kinacholindwa vizuri ni kuwa, inaweza kuonesha nia yake ya kulipiza kisasi, na kwa upande mwingine shambulizi dhidi ya kituo hicho halitaleta madhara mabaya kwa Marekani ili kuepuka vita rasmi.

    Hadi sasa Marekani haijatangaza vifo na majeruhi kutokana na mashambulizi hayo, lakini kuna habari kuwa ndege moja ya kijeshi na helikopta kadhaa za jeshi la Marekani zimeharibiwa.

    Baada ya kuuawa kwa Soleimani, viongozi wa Iran akiwemo Khamenei wamesema Iran italipiza kisasi dhidi ya Marekani kwa hatua kali. Rais Hassan Rouhani wa nchi hiyo jana alipozungumza kwa njia ya simu na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema, maslahi na usalama wa Marekani katika sehemu ya Mashariki ya kati ni tete, na haiwezi kuepuka matokeo ya kumwua Soleimani. Baraza la Usalama la Iran limesema, mipango 13 ya kulipiza kisasi kwa Marekani inafikiriwa, na hata mpango wenye hatari ndogo zaidi utakuwa "jinamizi ya kihistoria" kwa Marekani. Pia, bunge la Iran jana liliweka majeshi na wizara ya ulinzi ya Marekani kwenye orodha ya makundi ya kigaidi.

    Nchi nyingi za magharibi zina wasiwasi kuhusu ongezeko la mvutano. Ujerumani na Canada zimeamua kuondoa baadhi ya majeshi yao nchini Iraq.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako