• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mpango wa amani wa Mashariki ya Kati wa Trump wakosolewa

    (GMT+08:00) 2020-01-29 18:18:53

    Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza mpango wake wenye utata wa amani ya Mashariki ya Kati uliosubiriwa kwa muda mrefu, akitoa wito wa kuwepo kwa suluhu ya nchi mbili huku akiitambua Jerusalem kuwa mji mkuu usiogawanyika wa Israel.

    Trump alitoa mpango huo wenye kurasa 80 jana kwenye Ikulu ya White House mbele ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anayefanya ziara mjini Washington. Rais Trump ameutaja mpango huo kama ni fursa ya kuzinufaisha nchi zote mbili za Israel na Palestina, na kuongeza kuwa mji mkuu wa Palestina utajumuisha sehemu ya Jerusalem Mashariki. Amesisitiza kuwa Marekani kamwe haitaitaka Israel kuacha usalama wake.

    Baadaya kutolewa kwa mpango huo, rais Mahmoud Abbas wa Palestina ametangaza kuwa atabadilisha nafasi ya sasa ya Mamlaka ya Taifa ya Palestina, hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu hatua gani zitakazochukuliwa baadaye. Mamlaka ya Palestina ni serikali inayojiendesha iliyoanzishwa mwaka 1994 kufuatia makubaliano ya Gaza-Jericho ya kuongoza Ukanda wa Gaza na Maeneo ya A na B ya Ukingo wa Magharibi kama kutokana na Makubaliano ya Oslo ya mwaka 1993. Akiongea na wanahabari baada ya mkutano wa dharura wa viongozi mjini Ramallah, Ukingo wa Magharibi, rais Abbas amepinga kabisa mpango wa amani wa Trump na kusema mpango huo hautapitishwa na utaishia kwenye debe la taka. .

    Naye msemaji wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema Umoja huo utaendelea kuunga mkono watu wa Palestina na Israel kutatua mgogoro wao katika msingi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa, sheria ya kimataifa na makubaliano ya pande mbili, na kutambua dira ya nchi mbili zikiishi kwa amani na usalama katika misingi ya mipaka iliyotambuliwa kabla ya mwaka 1967.

    Wakati huohuo katibu mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu AL Ahmed Aboul-Gheit amesema suluhu zozote zile zitakazoletwa kwenye mgogoro kati ya Palestina na Israel hazitafanikiwa. Ameeleza kuwa mpango wa amani wa Mashariki ya Kati wa Marekani utajadiliwa kwenye mkutano wa dharura wa mawaziri wa baraza la jumuiya hiyo lakini kwa sharti la kuhakikisha maslahi ya nchi za kiarabu na Palestina. Na Umoja wa Ulaya umesema utasoma na kutathmini mpango huo, na ukisisitiza kuwa Umoja huo uko tayari kuitisha tena mazungumzo kati ya Israel na Palestina.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Hua Chunying amesema mpango wowote unatakiwa kusaidia suala la Palestina kutatuliwa kwa pande zote, haki na muda mrefu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako