• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Wataalam watoa wito wa kufanyiwa marekebisho ya Sheria ya Ulinzi wa Wanyamapori

  (GMT+08:00) 2020-01-31 21:03:30

  Kundi la wasomi nchini China limelitaka Bunge la Umma la China kufanyia marekebisho Sheria ya Ulinzi wa Wanyamapori ili kujumuisha usalama wa afya ya jamii katika matumizi ya bidhaa za wanyamapori. Wataalam hao wanataka kutungwa kwa sheria na kanuni mpya kuhusu wanyamapori. Wanasayansi na wasomi wanataka kuona mwisho wa biashara haramu na ulaji wa wanyamapori, na kusema yanahatarisha afya ya umma.

  Wataalam hao wamesema, chini ya kanuni zilizoko sasa, ni halali kufanya biashara, kusafirisha, kutengeneza na kuuza wanyamapori wasiolindwa ama bidhaa zao baada ya usajili na kupitishwa. Jambo hili linaloonekana kuwa shughuli ya halali mara nyingi inawafanya wanyamapori hao kuwa makazi ya magonjwa, na kuwa chanzo kikubwa cha maambukizi ya magonjwa "kutoka kwa mnyama kwenda kwa mnyama kwenda kwa binadamu na kwenda kwa binadamu".

  Mpaka sasa, wataalam kwa pamoja wametoa pendekezo kwa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China (CPPCC) kuhusu kufanya marekebisho na kuboresha sheria ya kuzuia ulaji wa wanyamapori haraka iwezekanavyo, na kutaka juhudi zaidi katika kanuni na utekelezaji wa sheria, kuzuia kwa pande zote wanyamapori na kubadilisha njia za maisha zisizo za kistaarabu. Wanasayansi wanaamini kuwa mlipuko wa virusi vya korona unahusishwa na biashara ya wanyamapori katika soko la samaki mjini Wuhan, jambo ambalo bado linachunguzwa.

  Wataalam hao wamesisitiza kuwa kudhibiti ama kufuta ulaji na biashara yao sio tu ni muhimu kwa ikolojia, bali pia kwa afya ya jamii. Wametoa wito kwa mamlaka za wanyamapori, taasisi za utekelezaji wa sheria na wasimamizi wa soko kuongeza juhudi kumaliza biashara haramu ya wanyamapori katika chanzo chake. Pia wamependekeza kuimarisha usimamizi, kujumuisha usalama wa afya ya jamii katika sheria ya ulinzi wa wanyamapori na kuboresha sheria zilizopo kuwakamata wanaokiuka sheria hizo.

  Baada ya mlipuko wa SARS mwaka 2003, iliyokuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Misitu ilichapisha orodha ya aina 54 za wanyamapori wa nchi kavu ambao wanaweza kutumika kibiashara na wale ambao teknolojia yao ya kuzaliana ilikuwa imekamilika. Aina hizo 54 kwa kiasi kikubwa zinatumika kwa chakula, dawa na manyoya.

  Sheria na kanuni zinazosimamia ulaji wa wanyamapori hazikubadilishwa mpaka mwaka 2016, wakati China ilipofanyia marekebisho sheria ya "Ulinzi wa Wanyamapori". Hata hivyo, ni wanyamapori walio chini ya ulinzi wa taifa pekee ambao wamezuiliwa kuliwa.

  Kutokana na mlipuko mpya wa virusi vya korona, China kwa mara nyingine tena inapambana na virusi vinavyoaminika kutokana na mnyama wa porini. Wakati huohuo, sheria imeendelea kubaki kama ilivyo. Wengi wanaamini kuwa, mlipuko huo unapaswa kutumika kama chanzo cha mabadiliko ya kuboresha kanuni.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako