• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China: Marekani imechukua hatua kupita kiasi kuhusiana na maambukizi ya korona

    (GMT+08:00) 2020-02-03 19:34:11

    China imeikosoa Marekani kwa kuchukua hatua kupita kiasi ambazo ni kinyume cha ushauri wa Shirika la Afya Duniani WHO kuhusiana na maambukizi ya virusi vipya vya korona.

    Miongoni mwa nchi kadhaa zilizowekea vikwazo raia wa China kuingia katika nchi hizo, Marekani ilipandisha ngazi ya hatari ya kwenda China kuwa ya juu kabisa na kuamua kuwa kuanzia jana, wageni wote waliokwenda China katika siku 14 zilizopita hawaruhusiwi kuingia Marekani.

    Akizungumzia hilo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bi. Hua Chunying amesema, nchi nyingi zimepongeza na kuunga mkono juhudi za China za kupambana na maambukizi ya virusi vipya vya korona, na China pia inaelewa na kuheshimu uamuzi wa nchi husika wa kuimarisha hatua za vipimo kwa raia wa China wanaoingia katika nchi hizo. Hata hivyo, hadi sasa, pamoja na kuwa haijatoa msaada wowote kwa China, Marekani imekuwa nchi ya kwanza iliyowaondoa wafanyakazi wa ubalozi wake mdogo mjini Wuhan, nchi ya kwanza iliyodai kuwaondoa baadhi ya wafanyakazi katika ubalozi wake mjini Beijing, na pia ni nchi ya kwanza iliyotangaza kuzuia kuingia kwa raia wa China nchini humo, hatua ambazo zimezusha na kueneza hofu duniani, ni mfano mbaya.

    Wakati huohuo, wizara ya afya ya Canada imeeleza wazi kuwa nchi hiyo haitaifuata Marekani kuwazuia Wachina na wageni waliokwenda China kuingia nchini Canada.

    Msemaji huyo ameongeza kuwa, tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi vya korona, serikali ya China imechukua msimamo wa kuwajibika na afya ya watu kwa kiwango cha juu, na kudhibiti na kuzuia kuenea kwa virusi kwa pande zote na kwa hali ya juu. Hatua hizo zimezidi jinsi inavyotakiwa kwa mujibu kanuni ya afya ya kimataifa, jambo ambalo mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO Bw. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, ni mfano wa kuigwa katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa kuambukizwa. Bw. Tedros amesema wazi kuwa kutangaza maambukizi ya virusi vipya vya korona kuwa "tukio la dharura la afya ya umma duniani" hakumaanishi kupiga "kura ya kutokuwa na imani" na China, na WHO ina imani na uwezo wa China kudhibiti maambukizi hayo, na hakuna sababu ya kuweka vikwazo dhidi ya usafiri na biashara dhidi ya China.

    Bi. Hua amesema China inatoa wito wa kuwepo kwa mtazamo sahihi, tulivu na kufanya maamuzi kwa njia ya kisayansi katika kukabiliana na maambukizi hayo. Ameongeza kuwa China inachukua msimamo wa uwazi na kuwajibika kwa kiwango cha juu, na kuimarisha ushirikiano na WHO na jamii ya kimataifa, na kusisitiza kuwa China ina imani na uwezo wa kushinda vita hivyo mapema.

    Wakati huohuo, Bi. Hua amesema tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi vipya vya korona, China imezingatia sana usalama wa maisha na afya ya raia wa nchi za nje walio hapa nchini, haswa wale walioko mjini Wuhan, Hubei. Pia imechukua hatua nyingi zenye ufanisi ikiwemo namba ya simu iliyo wazi kwa ajili ya kutoa taarifa na huduma kuhusu virusi vya korona, na kushughulikia matakwa yao halali kwa wakati.

    Kwa mujibu wa msemaji huyo, hadi jana tarehe 2, raia 16 wa kigeni waliopo hapa China wameambukizwa virusi vya korona, wawili kati yao wamepona na kutoka hospitali, na wengine 14 wanaendelea na matibabu kwa kuwekwa karantini na hali zao zinaendelea vizuri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako