Mchezaji wa timu ya Nasarawa United ya Ligi kuu ya Nigeria, Chieme Martins amefariki Jumapili jioni kiwanjani baada ya kuanguka. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya nchi hiyo, mshambuliaji huyo alidondoka wakati timu zote zikiwa bado hazijapata goli, baada ya kugongana na mchezaji wa timu pinzani katika mtanange mkali dhidi ya Katsina United uliopigwa kwenye uwanja wa Lafia Township jimboni Nasarawa. Madaktari wa timu walijaribu kuushtua moyo wake lakini hawakufanikiwa na kuita gari la wagonjwa lililopo uwanjani hapo ili kumuondoa uwanjani. Hata hivyo gari iligoma kuwaka na kusababisha kuchelewa kupata matibabu mapema kwa mchezaji huyo mwenye miaka 22. Imefahamika kuwa baadaye ilitumika gari ya wanahabari kumpeleka hospitali, lakini madaktari walishindwa kuokoa maisha yake na kutangazwa kufariki muda mfupi tu baada ya kufika hospitali. Hadi kipenga cha mwisho kinalia timu yake ya Nasarawe iliondoka ikiwa na magoli 3-0.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |