• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Afrika yapata vifaa vya kupambana na virusi vya Corona kutoka kwa Jack Ma wa China

    (GMT+08:00) 2020-03-23 18:20:42

    Wakati nchi za Afika zinafunga mipaka kutokana na hofu ya athari ya maambukizi ya virusi vya Corona, bilionea wa China ambaye ni mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Alibaba ya China, Bw. Jack Ma ameahidi kutoa vifaa vya upimaji zaidi ya milioni moja kwa bara hilo.

    Mpaka sasa bara hilo lenye idadi ya watu bilioni 1.3 limeripoti maambukizi karibu 1,100 katika nchi 43, na watu 39 kati yao wamefariki. Idadi hiyo ni sehemu ndogo katika idadi ya maambukizi ya watu 305,000 kote duniani.

    Taarifa iliyotolewa na mfuko wa Jack Ma inasema, kampuni hiyo haiwezi kupuuza hatari inayowezekana kutokea barani Afrika, na kufikiri bara hilo litaepuka ugonjwa huo, na dunia haiwezi kumudu matokeo mabaya ya maambukizi ya Corona barani Afrika.

    Jumapili, ndege ya shirika la ndege la Ethiopia iliyochukua mask milioni 5.4, vifaa vya upimaji milioni 1.08, mavazi ya kinga elfu 40 na ngao za uso elfu 60 zinazofadhiliwa na mfuko wa Jack Ma iliwasili Ethiopia kutoka Guangzhou, China.

    Rais Paul Kagame wa Rwanda kwenye ukurusa wake wa Twitter ameushukuru mfuko wa Jack Ma kwa kutoa vifaa vya upimaji wa virusi vya Conona. Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wiki iliyopita aliahidi kusambaza vifaa hivyo kwa nchi nyingine za Afrika.

    Mapema leo, Benki ya Dunia imesema imeahidi kutoa dola za kimarekani milioni 60 kwa Kenya ili kuisaidia kupambana na virusi hiyo.

    Katika nchi nyingine za bara hilo, kama vile Somalia ambayo inakabiliwa na mapigano, inaendesha vituo vyake vya afya ya umma kwa kutegemea wafadhili kutoka nchi za nje. Waziri wa Afya wa Somalia Fawziya Abikar Nur amesema wizara hiyo iliweka karantini na kuwapima wasomalia wanne ambao walirudi nchini humo kutokea China wiki iliyopita, na mmoja amethibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona. Wizara ya usafari wa anga imesema, safari za ndege za kimataifa kwenda Somalia zimesitishwa kwa muda wa wiki mbili. Hata hivyo, nchi hiyo jana ilifungua tena uwanja wake wa ndege kwa siku mbili ili kuwaruhusu raia wake kurudi kutoka nchi 14 zilizoathiriwa na virusi vya Corona. Raia hao watawekwa karantini watakapowasili uwanja wa ndege, na tayari makazi, vitanda na chakula vimeandaliwa.

    Wizara ya Afya nchini Tanzania pia imethibitisha kuwa, kuanzia ijumaa wiki iliyopita, kesi za maambukizi ya virusi vya korona imeongezeka kutoka sita mpaka 12 kufikia jana. Rais wa nchi hiyo John Magufuli amewataka wananchi kuwa makini zaidi na kufuatilia mwongozo unaotolewa na mamlaka za afya nchini humo. Pia mapema leo, Rwanda, Burkina Faso, Ethiopia, Senegal na Cameroon zote ziliripoti kuongezeka kwa kesi za maambukizi. Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini Tito Mboweni amesema nchi hiyo ambayo ina jumla ya kesi 274 za maambukizi ya virusi vya Corona, huenda itahitaji kuchukua fedha kutoka idara nyingine za serikali ili kupambana na ugonjwa huo.

    Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe Jumapili amewaambia waandishi wa habari kwamba ndege zote za abiria za kimataifa zitapigwa marufuku kuanzia Jumatano. Amesema ofisa wa kaunti ambaye alidhihaki sheria za karantini na kukutwa na maambukizi, atashitakiwa mara muda wake wa karantini utakapomalizika. Amesema wakenya ni lazima kutilia maanani suala hilo, na hatua zaidi zitatekelezwa wiki hii.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako