• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Nchi za Afrika zachukua hatua kukabiliana na virusi vya Corona

    (GMT+08:00) 2020-03-24 10:48:48

    Zimbabwe imefunga mipaka yake ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona. Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ametangaza hatua madhubuti za kupambana na virusi hivyo baada ya ugonjwa huo kusababisha kifo cha mtu mmoja.

    Rais Mnangagwa ametangaza hatua zinazoanza kutekelezwa mara moja, ikiwemo kufunga mipaka ya nchi hiyo kwa safari zote isipokuwa kwa mizigo na raia wanaorudi, na wakazi wanaorudi watatakiwa kufanyiwa upimaji na ufuatiliaji wa kimatibabu ikiwa ni pamoja na kujiweka karantini kwa siku 21, na kupiga marufuku shughuli za burudani, mikusanyiko, klabu za usiku, baa, majumba ya sinema, mabwawa ya kuogelea, viwanja vya mazoezi na shughuli za michezo.

    Wakati huohuo, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametangaza kwamba kuanzia Alhamisi wiki hii nchi nzima itafungwa kwa siku 21 ili kupambana na virusi vya Corona na kusema kukaa nyumbani, kufunga maeneo ya umma na kufuta shughuli zote za kijamii ni njia bora ya ulinzi dhidi ya virusi. Tangazo hilo linakuja baada ya idadi ya maambukizi kuongezeka kutoka 274 hadi 402.

    Rais Ramaphosa amesema maduka mengi yatafungwa isipokuwa kwa maduka ya dawa, maabara, benki, huduma muhimu za kifedha na malipo, pamoja na soko la hisa la Johannesburg JSE, vituo vya mafuta na vituo vya huduma ya afya.

    Rais Macky Sall wa Senegal ametangaza hali ya dharura ya taifa ili kukomesha kuenea kwa virusi vya Corona, ambapo watu 79 wameripotiwa kuambukizwa. Rais Sall pia amesisitiza kwamba serikali itachukua hatua zote muhimu kutekeleza hali ya dharura bila kuchelewa, pia ameagiza vikosi vya usalama kuwa tayari kwa utekelezaji wa haraka wa hatua zilizowekwa. Aidha amepiga marufuku watu kutoka nje kuanzia saa mbili jioni hadi kumi na mbili asubuhi, na kupiga marufuku mikusanyiko yote ya umma.

    Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria ameamuru watu kukaa nyumbani ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona katika mji mkuu Algiers na Jimbo la Blida. Uamuzi huo umefikiwa kwenye mkutano wa Baraza kuu la usalama uliofanyika ikulu. Hatua zilizotangazwa ni pamoja na watu kukaa ndani katika mkoa wa Blida kwa siku 10, kufungwa kwa maduka ya mikate na mboga, na kupiga marufuku mikusanyiko ya watu zaidi ya wawili.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako