• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Sekta ya maua nchini Kenya yapata pigo kufuatia maambukizi ya virusi vya CORONA

  (GMT+08:00) 2020-03-31 10:02:12

  Sekta ya biashara ya maua nchini Kenya imeathirika kutokana na kukosekana kwa soko la bidhaa hiyo kufuatia mlipuko wa maambukizi ya virusi vya CORONA CORONA.

  Wadau katika sekta ya biashara ya maua nchini Kenya wanasema mashamba mengi yanapata hasara kwa sababu yamepunguza usafirishaji wa bidhaa hiyo kwa kiwango kikubwa.

  Mwandishi wetu jijini Nairobi Khamis Darwesh ametuandalia ripoti ifuatayo.

  "Leo asilimia 100 ya maua yetu yanaharibiwa. Hakuna soko kwa hivyo maua yote tunayatupa jalalani"

  Huyo ni Sachin Apacchu, ambaye ni Meneja katika kampuni ya maua ya Bliss Flora Ltd, anasema maua yao yote sasa hivi yanaharibika kwa kukosa soko.

  Wakati janga la mlipuko wa ugonjwa wa CORONA likiathiri uchumi wa mataifa makubwa ulimwenguni, likisitisha usafiri wa ndege, mikusanyiko ya watu na shughuli za kawaida kila siku, sekta ya biashara ya maua nchini Kenya imenyauka.

  Badili ya kusafirishwa Ulaya au Mashariki ya kati ktumika kwa ajili ya harusi, misiba ya ishara za huba, maelfu ya maua sasa yanaishia kwenye jaa yanaharibika.

  Huku kukiwa na amri ya kutokuwa nje kuanzia saa moja jioni hadi 11 asubuhi nchini Kenya, kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa CORONA, biashara nyingi hivi sasa zinakadiria hasara kubwa.

  Amri hii haijatolewa Kenya tu bali nchi mbalimbali duniani, huku nyengine zikiwa na amri ya kutokuwa nje kabisa.

  Tangu kutokea kwa mlipuko wa maambukizi ya virusi vya CORONA, mojawapo ya sekta zilizoathirika pakubwa nchini Kenya ni sekta ya biashara ya maua.

  Kwa kiwango kikubwa sekta hii hutegemea kuuza mazao yake katika bara la Ulaya.

  Micah Cheserem ni mfanyabiashara anayefanya kilimo cha maua. Anasema hivi sasa hawauzi wala kusafirisha maua Ulaya kutokana na hali ngumu tangu mlipuko wa virusi vya CORONA.

  "Wateja wetu wengi Ulaya wamefuta oda zao. Sababu za wao kufuta oda zao ni kuwa wateja kule ulaya hununua maua barabarani au mitaani.Wauzaji maua huwa wako barabarani,kwa kawaida wateja huenda kununua maua pale wauzaji walipo, lakini kunapokuwa na amri ya kutotoka nje,hakuna yeyote anayeruhusiwa kwenda mitaani au barabarani"

  Cheserem anasema hivi sasa wadau katika sekta ya biashara ya maua wanapitia hali ngumu.

  "Hatujui hali hii itaendelea kwa muda gani, hatujui ni kipi kitatokea kwa wafanyakazi wetu kwa sababu hauwezi kuamka tu siku moja na kusema kwa sababu ya maambukizi ya virusi vya CORONA tutawafuta kazi."

  Idadi kubwa ya wafanyabiashara katika sekta ya biashara ya maua nchini Kenya wamesitisha kabisa usafirishaji wa bidhaa hii kutokana na ukosefu wa soko.

  Mkurugenzi wa Baraza la Maua nchini Kenya, Clement Tulezi anasema mlipuko wa CORONA umeiletea sekta hiyo hasara kubwa.

  "Soko letu kubwa liko Ulaya, ambako tuna asilimia 40 ya jumla ya soko la maua. Asilimia 70 ya uzalishaji wetu inakwenda Ulaya, kwa hivyo kitu chochote kinachotokea Ulaya kina athari ya moja kwa moja kwa kile tunachofanya"

  Kulingana na takwimu kutoka Baraza la Maua nchini Kenya, mauzo ya maua katika masoko ya nje hivi sasa yako chini ya asilimia 35 ya yale wanayotarajia katika kipindi kama hiki cha mwaka.

  Masoko ya Ulaya haswa Uingereza sasa yameshuka hadi sifuri.

  Katika mfumo wake wa uchumi wa kupambana na CORONA, Muungano wa Sekta Binafsi nchini Kenya (KEPSA) umezindua kampeni inayoitwa "Maua ya Matumaini".

  Kampeni hii itatekelezwa kupitia wanachama wa KEPSA kama vile Baraza la Maua nchini Kenya, Chama cha Waundaji Bidhaa nchini Kenya,Elgon Kenya,Shirika la Ndege la Kenya Airways na Jambojet.

  Kampeni hiyo ilianza jumatatu kwa usambazaji wa maua katika hospitali ya Taifa ya Kenyatta, Hospitali ya Mbagathi, Mama Lucy, hospitali ya Mathare, hospitali ya Uti wa Mgongo na Hospitali ya kujifungua kina mama ya Pumwani jijini Nairobi.

  Kampeni hii itaendelea katika sehemu mbalimbali za nchi katika siku zijazo.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako