• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Hatua zilizochukuliwa na mamlaka ya mji wa Mombasa katika kupambana na Corona

    (GMT+08:00) 2020-04-20 09:01:48

    Kaunti ya Mombasa nchini Kenya chini ya uongozi wake Gavana Hassan Ali Joho ni miongoni mwa majimbo yanayomulikwa kwa kila sababu nzuri wakati jimbo hilo likikabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona.

    Gavana Joho amepongezwa kwa kuwa msitari wa mbele akijaribu kuhakikisha kuwa mji wa Mombasa hauwi kitovu cha mlipuko wa ugonjwa huo, kwa kuweka mikakati kabambe ya kupambana janga la ugonjwa wa Corona.

    Mwandishi wetu Khamis Darwesh anatueleza mengi kuhusu juhudi zilizowekwa na kaunti ya Mombasa katika kupambana na Corona.

    Mji wa Mombasa ni wa pili kwa idadi ya visa vilivyothibitishwa vya maambukizi ya virusi vya Corona, baada ya mji mkuu Nairobi wenye visa vingi zaidi.

    Tangu mwanzo, ilipotambulika kuwa Mombasa pamoja na kaunti za Kwale na Kilifi ni maeneo ya hatari zaidi, Gavana Joho pamoja na Kamishna wa Kaunti ya Mombasa ambao wanasimamia kamati ya ugonjwa wa Corona ya kaunti hiyo, waliweka hatua kali za kuhakikisha watu wanatengana umbali wa mita moja ili kuzuia uambukizaji wa virusi hivyo.

    Tangu kutangazwa kwa ugonjwa wa Corona nchini Kenya, Mombasa ndio kaunti ya kwanza kupiga marufuku mtagusano wa watu katika vilabu, fukwe za bahari, saluni na maduka ya vinyozi-sehemu ambazo zinatajwa kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi.

    Aidha kaunti ya Mombasa imeweka mfuko wa kuwasaidia wasiojiweza na chakula cha msaada wakati huu wa ugonjwa wa Corona.

    "Serikali ya kaunti ya Mombasa imetenga Sh20om. Tumepewa ahadi za za msaada wa chakula kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani na sekta binafsi za thamani ya Sh100m na bado tunaendelea kukusanya misaada.Nina hakika serikali imeangalia michakato yote kuhusu gharama na usambazaji chakula na pia nayo inajitayarisha.Ikifika wakati kutangazwe amri ya kutotoka nje kabisa kutokana na ugonjwa wa corona nakuhakikishia kuwa hatutaruhusu watu wa Mombasa wafe njaa. Tutaingilia kati kama viongozi wao kuona ni kipi tunachoweza kufanya angalau kuwawezesha kulisha familia zao kwa kipindi ambacho watasalia nyumbani."

    "Ambacho tutatoa ni mfuko ulio na chakula, maji na madawa. Tutasambaza msaada huu katika nyumba zao. Tutaenda katika vitongoji duni vyote mjini Mombasa kwa kipindi chote watakachokuwa nyumbani. Marufuku ya kutotoka nje inaweza uamuzi mgumu sana kufanywa lakini hatutakomesha Corona ikiwa bado tutaendelea kuzurura na kuusambaza ugonjwa huo."

    Kufikia sasa kaunti ya Mombasa imeweza kukusanya msaada wa chakula kutoka kwa makampuni mbalimbali huku kukiwa na misaada ya chakula kutoka kwa watu binafsi, misaada ya vitakasa mikono na bidhaa nyenginezo.

    Wiki iliyopita, Gavana Joho pia alizindua vipumulio au vifaa vya kupumua 18 vilivyotolewa kama msaada na kiongozi wa falme ya kiarabu ya Dubai Sheikh Ahmed Mohamed Al Falas.

    Joho anasema lengo ni kuwa na vipumulio takriban 50.

    Katika kivuko cha Likoni, kwa ushirikiano kati ya Wakfu wa Suleiman Shahbal na Wakfu wa Hassan Joho kumejengwa vyumba vya vieuzi au vya kutakasa abiria wote kabla kuingia kwenye feri.

    Abiria wanatakiwa kuingia kwenye vyumba hivyo ambavyo vinanyunyiza vieuzi au sanitizer kupitia mabomba yaliyounganishwa kwenye vyumba hivyo.

    Gavana Joho anasema waliiagiza teknolojia hii kutoka China.

    "Serikali ya kaunti ya Mombasa iliona kuna umuhimu wa kuweka kifaa ambacho kitapima watu joto na pia kupiga picha. Kifaa hiki tulikiagiza kutoka Chinana tulipokiweka tuliweza kuona baadhi ya watu wanaovuka feri joto lao lilikuwa zaidi ya nyuzi joto 40."

    Zaidi ya abiria 300,000 na magari 6,000 hutumia kivuko cha Likoni kila siku.

    Vyumba kama hivi pia vimewekwa katika soko kuu la Kongowea mjini Mombasa na sehemu nyingine muhimu.

    Kwa uvumbuzi huu, Gavana Joho alimiminiwa sifa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na kuwataka magavana wengine kuiga mfano wake.

    Aidha wananchi kutoka sehemu mbalimbali za nchi wamemmwagia sifa Joho kwa uvumbuzi huu.

    Wiki iliyopita Gavana Joho alitangaza kuanzshwa kwa hospitali yenye vitanda 150 katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa wakati akiitayarisha kaunti hiyo, endapo visa vya wanaopata maambukizi ya Corona vitaongezeka.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako