• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mikakati ya nchi za Afrika Mashariki katika kupambana na kuenea kwa janga la Corona

    (GMT+08:00) 2020-05-04 09:15:28

    Serikali mbalimbali barani Afrika zinaendelea na jitihada za kutekeleza sera ya kukabiliana na ugonjwa wa Corona.

    Nchi zinaendelea kufuata maagizo yaliyotolewa na Shirika la Afya Duniani ya kujikinga na Corona pia nchi hizo zikiweka mikakati mengine ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi hivyo.

    Katika juhudi za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Corona serikali mbali mbali za bara la Afrika zimetangaza hatua ya kufunga miji au nchi kwa maana ya kwamba shughuli za kawaida za kimaisha haziruhusiwi tena kufanyika au baadhi ya nchi zimetangaza kuzuia watu kutoka nje, na zile ambazo zimeruhusu raia wake wamekuwa waoga na hata wengine kulazimika kufunga biashara zao.

    Hatua kuu zilizofanyika Afrika Mashariki ili kupunguza kusambaa kwa maambukizi ni pamoja na akufungwa kwa taasisi zote za elimu,nyumba za kulala wageni,migahawa,makanisa,misikiti,ofisi za umma na binafsi,vyombo vya usafiri,viwanja vya michezo,taasisi za fedha,sehemu za starehe na masoko.

    Rwanda ilitangaza kulegeza vikwazo kiasi,imefungua tena nchi na kuanzia leo tarehe 4 Mei imeruhusu watu kwenda kazini katika juhudi za kufufua uchumi wa nchi.

    Biashara za umma na binafsi zitarejelea shughuli hii leo na wafanyakazi muhimu zaidi huku wengine wakiendelea kufanya kazi wakiwa nyumbani.

    Waziri Mkuu Edouard Ngirente alisema sekta ya viwanda na ujenzi zitaruhusiwa kufanya kazi na wale wafanya kazi muhimu zaidi.

    Masoko hayatazidi asilimia 50 ya wauzaji wote.Hoteli na migahawa itafungua na kufunga kufikia saa 1 jioni,lakini mikusanyiko ya watu wengi bado imepigwa marufuku.

    Rwanda ilitangaza kufungwa kabisa kwa nchi hiyo na wananchi kutotoka nje kwa muda wa wiki mbili tarehe 21 Machi wakati ilipopata visa vya kwanza vya maambukizi ya Corona.Muda huo uliongezwa tena hadi tarehe 30 Aprili.

    Katika mkutano wa Baraza la Mawaziri nchini Uganda,ulioongozwa na Rais Yoweri Museveni ,baraza hilo lilikubaliana kwamba kila sekta ya serikali iunde mpango wa kuifungua tena nchi kwa awamu.

    Rais Museveni alisema hatua kali zimesaidia kudhibiti uenezaji wa ugonjwa wa Corona nchini humo.

    Amri ya kutotoka nje nchini humo inafaa kukamilika kesho.

    Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa anasema wanaendelea kutoa maagizo na kuchukua hatua kila wataalamu wao wanapofanya tathmini na kuishauri serikali.

    "Sisi Tanzania tumepata tatizo hili na tunaendelea kupambana nayo ili kuzuia maambikizi yasije yakazagaa nchi nzima.Tumezuia mikusanyiko ,tumeeimisha watu kukaa mbali wanapopata huduma,lakini pia tunajitahidi kupeleka elimu mpaka vijijini watu wanawe mikono,wapake dawa za kuua vijidudu mikononi,na maelekezo tunaendelea kuyatoa kila siku kadri hali inavyokwenda.Sisi tunafanya tathmini ya ugonjwa huu kila siku na wataalamu wako bize,na hatua hizi tutazichukua kadri wataalamu wetu wanavyoendelea kufanya tathmini na kuishauri serikali"

    Wananchi wametakiwa kwenda kwenye vituo vya afya iwapo wataonyesha dalili za ugonjwa wa Corona.

    Nchini Kenya serikali ilitangaza zuio la watu kutoingia na kutoka ndani ya kaunti za Nairobi,Mombasa,Kwale na Kilifi.

    Vilevile pia Kenya kumetangazwa amri ya kutokuwa nje kuanzia saa 1 usiku hadi saa 11 asubuhi.

    Hata hivyo kumekuwa na visa vya baadi ya watu kutotii amri hii,huku wengine wakikamatwa na kupelekwa kwenye vituo vya karantini.

    Katika kikao cha kutoa takwimu za wagonjwa wa Corona jana,Katibu Mkuu wa Utawala katika Wizara ya Afya nchini Kenya Dkt Rashi Aman alisema watu wote watakaokiuka amri hii watakamatwa na kutengwa katika vituo maalum vitakavyoundwa kwa ajili yao.

    "Kuhusu karantini,kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu hali ya wanaokamatwa wakikiuka sheria za amri ya kutotoka nje.Ningependa kusema kuwa watu hao hawatawekwa katika vituo vya serikali vya karantini,na badala yake Inspekta Mkuu wa Polisi ameelekezwa na Kamati ya Kitaifa majanga kuunda kituo cha wanaovunja sheria za amri ya kutotoka nje.Kituo hicho kinafaa kuzingatia mahitaji ya watu kutengana kwa umbali wa mita moja na nusu"

    Waziri wa Afya Zanzibar,Hamad Rashid aliwaomba wananchi wanaowekwa karantini kutoona kama ni mateso bali ni kwa ajili ya kuwalinda wengine kutokana na maambukizi.

    "Serikali inapochukua hatua ya kukuweka kambini siku 14 na tunakupima na kukuchunguza,hata kama umepona bado tunaendelea kukuchunguza ni halali kabisa,ni haki kutokana na asili ya virusi hivi.Serikali haina nia ya kumuweka mtu kambini ikamtesa lakini nia yetu ni kutaka usalama wa nchi yetu

    Vifo viliyosababshwa na maambukizi ya virusi vya Corona duniani kote vimepita 230,000 kufikia mwishoni mwa wiki huku idadi ya visa vya wanaougua ugonjwa huo vikifika zaidi ya milioni 3.

    Kwa ujumla virusi vya maambukizi ya ugonjwa wa Corona vimesambaa katika nchi na maeneo 187.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako