• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kenya yafunga mipaka yake na Tanzania,Somalia ili kudhibiti usambaaji wa Corona

    (GMT+08:00) 2020-05-18 09:30:04

    Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta jumamosi alitoa agizo la kufungwa kwa mipaka ya nchi hiyo na Tanzania na Somalia kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Corona mipakani.

    Rais Kenyatta aidha aliongeza muda wa zuio la kuingia na kutoka ndani ya kaunti za Nairobi,Mombasa,Kwale,Kilifi na Mandera kwa siku 21 zaidi ili kudhibiti maambukizi ya corona kutoka kaunti moja kwenda nyingine.

    Mwandishi wetu Khamis Darwesh ametuandalia ripoti ifuatayo.

    "Kufuatia ushauri kutoka kwa kamati ya kitaifa ya kushughulikia maambukizi ya virusi vya corona na Baraza la Usalama la taifa,leo natoa maagizo yafuatayo:kuwa kutakuwa na zuio la watu na abiria wowote,magari ya abiria ,kuingia na kutoka katika mipaka ya Kenya kupitia mpaka wa Kenya na Tanzania,isipokuwa kwa magari ya kubeba mizigo tu kuanzia leo jumamosi tarehe 16 Mei saa sita usiku.Na pia agizo hilo nimelitoa kwa mipaka kati ya Kenya na Somalia,isipokuwa tu kwa magari ya mizigo.Agizo litaanza kutekelezwa leo jumamosi tarehe 16 Mei kuanzia saa sita usiku"

    Rais Kenyatta pia alitoa agizo la madereva wote wa magari ya kubeba mizigo kufanyiwa vipimo vya lazima vya Corona,na kuruhusiwa kuingia nchini iwapo tu watapatikana hawana ugonjwa huo.

    Wakati akihutubia taifa siku ya jumamosi,Rais Kenyatta alisema kufungwa kwa mipaka kumesababishwa na kupatikana visa vingi vya Corona kutoka nchi jirani.

    "Miongoni mwa waliopatikana na Corona nchini Kenya wiki hii iliyopita,jumla ya visa 43 ni vya waliovuka mpaka kutoka nchi jirani za Somalia na Tanzania.Kufikia ijumaa iliyopita kesi za waliovuka mipaka ni kama ifuatavyo :Wajir ilikuwa na visa 14 vya mpakani,Isebania 10,Namanga 16 ,Lungalunga 2,na Loitoktok 1.Visa hivi 43 vinawakilisha takriban robo ya visa 166 vya maambukizi vilivyothibitishwa wiki iliyopita"

    Wakati huo huo Rais Kenyatta alitoa agizo la kuendelea kwa amri ya kutokuwa nje kuanzia saa 1 usiku hadi saa 11 alfajiri nchini kote.

    "Amri ya kutokuwa nje kuanzia saa 1 usiku hadi 11 alfajiri inayoendelea nchini itaongezwa kwa siku 21 zaidi hadi tarehe 6 Juni,na pia zuio la watu kuingia na kutoka nje ya kaunti za Nairobi,Kilifi,Mombasa,Kwale na Mandera pia litaongezwa muda hadi tarehe 6 Juni"

    Kufikia jumamosi Kenya ilikuwa na visa vipya 49 na kufikisha idadi ya watu wote walioambukizwa corona kuwa 830.

    Watu watano zaidi walifariki na kufikisha idadi ya walioaga kuwa 50.

    Rais Kenyatta alisema watu 300 ambao walikuwa wakitibiwa katika vituo mbalimbali wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

    Hata hivyo alisema bado kuna wengine 481 wanaoendelea kupata matibabu katika vituo mbalimbali vya kujitenga nchini kote.

    Pia Rais Kenyatta aliwashukuru na kuwapongeza wahudumu wa afya kwa kujitolea kwao katika kupambana na janga la Corona.

    Kufikia jana jumapili ,Kenya iliandikisha visa vipya 57 vya maambukizi ya virusi vya Corona na kufanya nchi kuwa na jumla ya visa 887 na vifo 50.

    Duniani kote watu zaidi ya 300,00 wameaga dunia kutokana na Corona,huku zaidi ya watu milioni 4.7 wakipata maambukizi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako