Wataalam wengi wameikosoa barua iliyoandikwa na rais wa Marekani Donald Trump kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk. Tedros Ghebreyesus.
Katika barua hiyo, rais Trump ametishia kuwa Marekani itaondoa ufadhili wake kwa Shirika hilo kama halitafanya maboresho dhahiri ndani ya siku 30 zijazo.
Profesa Lawrence Gostin wa sheria ya kimataifa ya afya na mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Sheria ya Afya ya O'Neill iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Georgetown ameandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa, kwa uhalisi barua hiyo haikupaswa kuandikwa. Profesa huyo ameuliza uwezo wa rais Trump kutoa vitisho hivyo, na kusema bunge la Marekani halitakubali kujitoa kwenye Shirika hilo.
Mhadhiri wa elimu ya usalama wa taifa katika jopo la washauri bingwa la Baraza la Uhusiano wa Kigeni nchini Marekani Bw. Max Boot amesema, kutishia kujitoa WHO wakati wa mgogoro wa kiafya duniani ni siasa za kijiografia ambazo ni sawa na kuchoma sindano yenye dawa Clorox kama tiba ya virusi vya Corona. Ameongeza kuwa, Marekani iliamua kushughulikia mlipuko huo peke yake na imeshindwa vibaya katika kupambana na janga hilo, na kusema hilo ni kosa la rais Trump, na sio WHO.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |