Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) limepanga Agosti 20 kuwa siku ya mwisho ya kukamilika kwa Ligi Kuu ya Serie A msimu huu huku kampeni za msimu mpya wa 2020-21 ukitazamiwa kuanza rasmi mnamo Septemba 1, 2020. Hadi kivumbi cha Serie A kiliposimamishwa kwa muda Machi 2020 kutokana na janga la corona, kila kikosi kilikuwa kimesalia mechi 12 za kucheza katika kampeni za msimu huu. Mabingwa watetezi Juventus wanaofukuzia ufalme wa taji la Serie A kwa mara ya tisa mfululizo msimu huu, wanaselelea kileleni mwa msimamo wa ligi kwa alama 63, moja zaidi kuliko Lazio ambao ni wa pili. Kwa mujibu wa FIGC, iwapo ligi yoyote kati ya tatu za madaraja ya juu nchini Italia itasitishwa baada ya kuanza tena, basi washindi wa kila ligi na wale watakaoshushwa daraja mwishoni mwa msimu huu wataamuliwa kwa njia ya mchujo. Iwapo itakuwa vigumu kwa ligi hizo kukamilika kupitia mchujo, basi washindi wataamuliwa kwa matokeo yatakayokuwa yamesajiliwa na kila kikosi hadi kufikia wakati wa kusimamishwa tena kwa kampeni za msimu huu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |