Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Biashara, Viwanda na Ushindani nchini Afrika Kusini Bw. Lionel October amesema, hatua ya kuifunga nchi hiyo kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona imetimiza lengo lake, na kwamba huu ni wakati wa kufungua uchumi wa nchi hiyo licha kuongezeka kwa maambukizi ya virusi hivyo.
Akitoa taarifa mbele ya Kamati ya Mawaziri ya Bunge la nchi hiyo kuhusu Biashara na Viwanda juu ya hatua za kufungua uchumi, Bw. October amesema serikali inahitimisha mashauriano na wadau mbalimbali kuhusu jinsi ya kufungua tena viwanda kwa utaratibu na kuanza tena uzalishaji.
Amesema sehemu kubwa ya uchumi inatarajiwa kufunguliwa tena wakati nchi hiyo ikielekea kwenye ngazi ya tatu ya zuio mwezi ujao.
Mpaka kufikia jana, Afrika Kusini iliripoti kesi mpya 1,134 za maambukizi ya virusi vya Corona, ikiwa ni kiasi cha juu zaidi kwa siku tangu kesi ya kwanza ilipotangazwa mwanzoni mwa mwezi Machi, na kufanya idadi ya jumla ya kesi za maambukizi kufikia 19,137, ikiwa ni ni ya juu zaidi barani Afrika.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |