• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Idadi kubwa ya wakenya wanaugua maradhi yasiyoambukiza (NCD)

    (GMT+08:00) 2020-06-15 09:34:35

    Waziri wa Afya nchini Kenya, Mutahi Kagwe jana alisema ugonjwa wa Corona sio unaoiumisha serikali kichwa lakini idadi kubwa ya magonjwa yasiyoambukiza ndio jambo linaloitia serikali wasiwasi.

    Kagwe alisema ni jambo la kutia wasiwasi kuwa katika kila vifo vitatu kimoja kinatokana na maradhi yasiyoambukiza na kwamba nusu ya watu waliolazwa hospitalini nchimi Kenya ni kutokana na magonjwa yasiyoambukiza.

    "Vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza vinaongezeka kwa haraka na kusababisha mzigo mara mbili wa magonjwa na kulemaza mifumo yetu ya afya.Magonjwa yasiyoambukiza yanachangia kifo kimoja katika kila vifo vitatu na vinachangia nusu ya watu waliolazwa hospitali nchini kwetu"

    Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe ameeleza wasiwasi huku kuongezeka kwa idadi ya magonjwa yasiyoambukiza nchini Kenya.

    Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Nyeri,kagwe alisema ugonjwa wa Corona sio ugonjwa pekee unaoitia wasiwasi serikali lakini pia ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.

    Alisema wagonjwa wanaougua maradhi yasiyoambukiza wako katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa Corona.

    Kagwe alisema idadi kubwa ya watu wanaugua maradhi yasiyoambukiza kama vile shinikizo kubwa la damu,kisukari na saratani.

    Alisema idadi ya wagonjwa hao inatarajiwa kuongezeka zaidi.

    "Vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza vinakadiriwa kuongezeka hadi asilimia 55 kufikia mwaka 2030,isipokuwa kama hatua sahihi za uangalifu endelevu kuhusu kuzuia na utunzaji zitafanywa.Magonjwa yasiyoambukiza yanatambulika kuwa na uwezo wa wa kumfanya mtu na majumba mengi kuingia kwenye umaskini kutokana na gharama za juu za utunzaji .Pia inakadiriwa kuwa yanaweza kupunguza mapato kwa asilimia 30.Nina wasiwasi kuwa karibu na asilimia 24 ya idadi yote ya watu kenya inaishi na shinikizo kubwa la damu ilhali asilimia 5 wanaugua kisukari"

    Fauka ya hayo,Kagwe alitoa wito kwa wananchi kufanya vipimo mara kwa mara ili kuepuka gharama kubwa za kutibu magonjwa haya wakati yanapokuwa yashakomaa bila kutambulika mapema.

    "Magonjwa haya kwa kawaida yanaua taratibu bila kuonyesha dalili zozote kwa miaka mingi hata kama ugonjwa huo unafika hatua ya juu.Mara nyingi dalili hazitaonekana isipokuwa tu kama tutafanya vipimo mara kwa mara.Katika visa vingi wakati mtu anapoonyesha dalili ,ugonjwa huwa ushafika hatua mbaya sana,na hatari ya kupata mshtuko wa moyo au kiharusi inaongezeka zaidi.Hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa ugonjwa unapotambulika mapema ni za gharama nafuu kuliko ugonjwa unapotambulika wakati ushasambaa kwa kiwango kikubwa"

    Takwimu zinaonyesha kuwa watu 47,000 hupatikana na saratani nchini Kenya ,na 32,000 hupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

    Waziri Kagwe alisema kaunti ya Nyeri ambayo ni miongoni mwa maeneo yenye magonjwa mengi yasiyoambukiza ina viwango vya visa 700 vipya vya saratani kila mwaka, na nusu ya vifo vinavyoripotiwa humo vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza.

    Aidha Kagwe alisema serikali katika sera yake ya uzuiaji na udhibiti inalenga kushirikiana na serikali za kaunti kufanya uhamasisho kuhusu maradhi yasiyoambukiza.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako