Mashabiki na wapenzi wa Liverpool wamelianzisha kila mtaa kushangilia ubingwa. Tangu Liverpool kutangazwa mabingwa, mashabiki wa mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu England, hawalali wala kufanya kazi ni kushangilia mitaani tu. Jambo hilo limeanza kuwapa hofu watawala na kutangaza hali ya hatari. Makundi makubwa ya mashabiki yamekuwa yakizunguka kwenye mitaa mbalimbali na kusababisha uchafuzi wa mazingira na sasa mamlaka imeonya kwamba, itaanza kuchukua hatua mbadala kuwadhibiti. Taarifa zinaeleza kuwa, Mamlaka za Serikali zimeonya kuwa kama hali hiyo itaendelea basi Liverpool itapigwa marufuku kutumia Uwanja wa Anfield kwenye mechi zake za Ligi Kuu England zilizobaki. Hatua hiyo ambayo imeungwa mkono na Polisi na hata klabu inalenga kuhakikisha hali ya utulivu inarejea kama zamani kwani, mashabiki hao wamesahau kama kuna janga la corona na maelekezo ya wataalamu wa afya ni lazima wafuatwe. Polisi wa Merseyside na Meya wa Jiji hilo, Joe Anderson, kwa nyakati tofauti wamekemea vitendo vinavyoendelea kwa mashabiki hao kwamba, vinakiuka tahadhari za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona. Kwa maana hiyo, mamlaka hizo zinakusudia kufuta kwa muda leseni ya matumizi ya Anfield kwa sababu za kiusalama kama mashabiki hao hawatakoma kushangilia kwa kuandamana mitaani. Liverpool bado wana mechi saba mkononi na kati ya hizo tatu itakipiga kwenye dimba la nyumbani, Anfield ikiwemo ile ya Aston Villa, Burnley na Chelsea ambao waliwapa taji kwa kuwachapa Man City.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |