• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Ujenzi wa daraja la watu pekee waanza Likoni

  (GMT+08:00) 2020-08-07 18:34:02
  Msongamano katika kivuko cha Likoni nchini Kenya unatazamiwa kupungua hivi karibuni kufuatia kuanza kwa ujenzi wa daraja la watu pekee ambalo linajengwa kwa gharama ya Sh1.5 bilioni.

  Ujenzi wa daraja hilo la kuelea umeanza eneo la Liwatoni upande wa Mombasa kisiwani na utamalizikia upande wa Likoni eneo la Peleleza.

  Kazi imeanza kwa wiki moja sasa baada ya tume ya ardhi ya NLC kuchukua ardhi kutoka kwa wamiliki wa eneo hilo la Liwatoni baada ya mashauriano.

  Mradi wa daraja hilo unatazamiwa kupambana na msongamano wa mara kwa mara katika kivuko cha Likoni ambacho kinatumiwa na watu zaidi ya 320, 000 kwa siku.Misongamano ya watu na magari imekuwa ikishuhudiwa kwa sababu ya kuharibika kwa feri kivukoni hapo.

  Hivi majuzi, watu zaidi ya 20 walijeruhiwa baada ya mkanyagano uliosababishwa na kuondolewa kwa feri mpya ya Mv Safari.

  Feri hiyo ya Mv Safari iliondolewa baada ya kugongwa na ile ya Mv Kwale. Kufikia sasa feri hiyo ya Mv Safari haijarudishwa kazini.

  Msimamizi wa sehemu ya ujenzi huo Bw Evans Momanyi amesema kuwa sehemu ambayo itashikilia vyuma vya daraja hilo utamalizika mwisho wa mwezi huu. Daraja hilo litakuwa na upana wa mita sita na urefu wa mita 529 na kutoka upande wa Mombasa kisiwani na kuvuka bahari hadi upande wa Likoni. Katikati ya daraja hilo kutakuwa na sehemu ambayo inafunguka ili kuruhusu meli na vyombo vyingine vya baharini kupita.Meli zinazoingia bandarini Mombasa hutumia sehemu hiyo ya kivuko cha Likoni ambapo daraja hilo litawekwa. Zaidi ya watu 10,000 watalazimika kutumia feri ya upande wa Likoni, ambako tayari zaidi ya watu 300,000 husongamana kila siku.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako