• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Nchi za Afrika zatarajia kutumia fursa ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya huduma kukuza ushirikiano na China kwenye sekta ya utalii

    (GMT+08:00) 2020-09-08 18:14:29

    Afrika ina raslimali nyingi za utalii, na sekta ya utalii pia imekuwa moja ya nguzo kuu za uchumi wa nchi nyingi za Afrika. Wakati sekta hiyo imeathirika vibaya na janga la virusi vya Corona kote duniani, nchi za Afrika zinatarajia kutumia fursa ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Huduma ya China kuwavutia watalii wengi zaidi wa China kuzitembelea nchi hizo.

    Kwenye banda la Angola katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Huduma ya China yaliyofunguliwa Septemba 4 mjini Beijing, mfanyakazi Jose Andrade amewaambia wanahabari kuwa Angola ikiwa ni moja ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi barani Afrika, uchumi wake unategemea sana biashara ya mafuta. Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Angola imeweka sera ya kuhimiza uchumi anuwai na kujitahidi kutafuta vichocheo vipya vya ukuaji wa uchumi. Amesema Angola inatarajia kutumia fursa ya maonesho hayo kutangaza raslimali zake za utamaduni na utalii. Balozi wa Angola nchini China Bw. Joao Savador dos Santos Neto amewaambia wanahabari wetu kuwa, kushiriki kwenye maonesho hayo kutasaidia kuwafahamisha wachina wengi zaidi kuhusu Angola.

    "Tumefanya maonesho kuhusu utamaduni na utalii wa Angola, na kuwaonesha watu wa China kuhusu upande mwingine wa nchi yetu. Maonesho haya ni mazuri sana, ni fursa nzuri kwetu kuwafahamisha watazamaji wa China kuhusu raslimali za utalii za Angola na hali ya jumla ya nchi yetu. Pia tumeleta vipeperushi, ili watazamaji waweze kuvichukua na kupata taarifa zaidi kuhusu Angola."

    Takwimu zilizotolewa na Baraza la Usafiri na Utalii Duniani WTTC zinaonesha kuwa, mwaka 2019 sekta ya utalii ilileta mapato ya dola za kimarekani bilioni 170 kwa uchumi wa Afrika, na kuleta fedha za kigeni na kutoa mamilioni ya nafasi za ajira kwa nchi za Afrika. Janga la virusi vya Corona limetoa pigo kubwa kwa sekta ya utalii katika nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Botswana. Kwenye maonesho hayo, Ubalozi wa Botswana nchini China pia umeleta vipeperushi kuhusu utalii wa Botswana, ikitarajia kuwafahamisha watalii wengi zaidi wa China kuhusu Botswana. Ofisa mwandamizi wa Ubalozi huo Bw. Emmanuel Pheko amesema:

    "Kutokana na athari za janga la virusi vya Corona kwa safari za kimataifa, mapato yanayotokana na sekta ya utalii nchini Botswana yamepungua kwa kiasi kikubwa. Tunajua watalii wa China wanapenda kutembelea nchi za nje, pia tunatumai kuwavutia kuja Botswana. Tunatarajia kutumia fursa ya maonesho haya kuwasiliana na wachina wengi zaidi, kuwafahamisha kuhusu vivutio vya utalii nchini Botswana, na tunatumai kuwa watakuja kuitembelea nchi yetu baada ya janga la virusi vya Corona kumalizika."

    Sekta ya utalii ni chanzo kikubwa zaidi cha fedha za kigeni nchini Rwanda. Mwanzoni mwa mwezi Agosti, Rwanda ilipewa cheti cha usalama na Baraza la Usafiri na Utalii Duniani WTTC, na uwanja wa ndege wa Rwanda pia umefunguliwa tena kwa wasafiri wa kimataifa kuanzia Agosti mosi. Kwenye maonesho hayo, konsela wa biashara katika Ubalozi wa Rwanda nchini China Bw. Samuel Abikunda ametoa mwaliko kwa watalii wa China kwa kutumia lugha ya kichina.

    "Wachina husema 'milima ya kijani na maji safi ni sawa na milima ya dhahabu na fedha', kwetu nchini Rwanda pia kuna milima na mito yenye mandhari nzuri. Rwanda ina wanymapori mbalimbali kama vile Simba na Twiga, lakini pia ina wanyama maalumu ambao hawapo katika nchi nyingine, kama vile Sokwe wakubwa wa milimani, huenda ni nchini Rwanda pekee tunaweza kuona jamii nzima ya Sokwa wakubwa. Hivi sasa Rwanda imefungua tena shughuli za utalii, na pia imepewa Cheti cha Usalama na Baraza la Usafiri na Utalii Duniani WTTC. Ningependa kuwaambia kwamba ni salama sana kutembelea Rwanda, tunaweza kufunga safari hata sasa hivi."

    Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya watalii wa China wanaotembelea nchi za Afrika imeongezaka kwa kasi, kwa hivyo ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye sekta ya utalii hakika utakuwa na mustakbali mzuri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako