• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • SOKA: Neymar na ndoto zake za kuwakimbilia Pele na Ronaldo

    (GMT+08:00) 2020-10-14 17:57:44

    Neymar Junior, alifunga magoli matatu katika ushindi wa 4-2 ulioupata Brazil, dhidi ya Peru katika muendelezo wa michezo ya kufuzu kucheza fainali za kombe la Dunia 2022. Nyota huyo wa PSG ya nchini Ufaransa sasa amefikisha magoli (64), akimzidi Ronaldo de Lima ambaye amefunga magoli (62), katika orodha ya wafungaji wa muda wote wa kikosi cha Kijani na Manjano. Mpaka sasa rekodi ya mfungaji bora wa muda wote katika timu ya taifa ya Brazil, inashikiliwa na Pele mwenye magoli (77).

    Neymar, ana umri wa miaka (28) anatazamiwa kuivunja rekodi ya Mfalme wa soka duniani, kutokana na anaoshindana nao wote kuwa wameshastaafu kucheza soka. Kitu pekee kinachomnyima mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona, heshima nchini kwake ni kushindwa kung'aa katika mashindano makubwa anapovaa jezi za Celecao.

    Edson Arantes do Nascimento (Pele), alitwaa ubingwa wa kombe la dunia mara tatu, Ronaldo Luis Nazario de Lima, amefanya hivyo mara mbili 1994 Marekani na 2002 Korea Kusini na Japan. 2014, mashindano hayo makubwa ya soka duniani yalifanyika nchini Brazil, Neymar alitazamiwa kuiongoza Celecao kutwaa ubingwa wao wa kwanza tangu 2002, lakini aliumia katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Colombia na kuzima ndoto za taifa hilo kutwaa kombe katika Ardhi ya nyumbani.

    Nchini Urusi mwaka 2018 Neymar hakuwa katika ubora uliozoeleka alikuwa kivuli cha mchezaji aliyesajiliwa kwa pesa nyingi katika uhamisho wake wa kutoka Barcelona kwenda PSG mwaka 2017, safari yao iliishia mikononi mwa timu ya taifa ya Ubelgiji hatua ya robo fainali.

    Mashindano ya 2022 yatatoa nafasi nyingine kwake kukiongoza kikosi cha Manjano na Kijani, kushinda kombe la dunia na kujiwekea heshima kama ni mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea katika taifa hilo, ambalo linaishi na kupumua mchezo wa mpira wa miguu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako